WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa Julai 27, 2025 amewasili mjini St. George’s, nchini Grenada ambapo
atamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Jukwaa la nne wa Kibiashara
na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (Afri-Caribbean Trade and Investment Forum
- ACTIF 2025) unaotarajiwa kufanyika Julai 28–30, 2025 katika kituo cha
mikutano cha Radisson.
Mkutano huo mkubwa
unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa ya Afrika na
visiwa vya Karibiani una kaulimbiu inayosema: “Uhimilivu na Mabadiliko:
Kuimarisha Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Afrika na Karibiani katika Kipindi
cha Changamoto za Kidunia.”
Katika mkutano huo,
Waziri Mkuu anatarajiwa kushiriki mjadala wa Mjadala wa Wakuu wa Nchi na
Serikali, kukutana na viongozi wa mataifa mengine, pamoja na kushiriki katika
mikutano ya uwili na wawekezaji wakubwa, ikiwa ni dhamira ya Tanzania ya
kuendeleza juhudi zake za kuvutia wawekezaji wa kimataifa ili kusaidia katika
kujenga uchumi wa kisasa na shindani duniani.
Ushiriki wa Mheshimiwa
Majaliwa katika mkutano huo akimwakilisha Rais Dkt. Samia ni mwendelezo wa
dhamira ya dhati ya kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuifungua nchi
kimataifa na kuimarisha ushirikiano, ili kuchochea maendeleo jumuishi kwa
Watanzania wote.
Baadhi ya maeneo muhimu
ambayo yatajadiliwa katika mkutano huo ni kuanzishwa kwa eneo la Biashara Huria
kati ya Afrika na Karibiani, kuimarisha baraza la biashara la Afrika na
Karibiani, kuchochea uchumi na ubunifu pamoja na Kukuza uhusiano wa usafiri wa
anga na baharini kati ya Afrika na Karibiani.
Mkutano huo umeratibiwa
na Jamhuri ya Granada pamoja na taasisi ya kifedha ya kimataifa yenye lengo la
kukuza biashara ya bidhaa na huduma ndani na nje ya Afrika (Afreximbank).
0 Maoni