Ubalozi wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania nchini Sweden ukishirikiana na jumuiya za Watanzania
waishio nchini humo, umeandaa na kufanikisha sherehe za maadhimisho makubwa ya
Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika tarehe 5 Julai, 2025, jijini
Stockholm.
Maadhimisho haya
hufanyika duniani tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuanzia mwaka 2022 kufuatia
azimio lililopitishwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa
Mataifa (UNESCO).
Akizungumza katika
maadhimisho hayo, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, amesema
kuwa Serikali imeazimia kukieneza na kukienzi Kiswahili duniani kote huku
akielezea namna kilivyosambaa na kuongeza kuwa kwa ushawishi wa Tanzania,
Kiswahili sasa ni lugha ya kikazi Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mgeni rasmi katika
maadhimisho hayo alikuwa Waziri wa zamani wa Usawa na Jinsia nchini Sweden,
Mhe. Nyamko Sabuni, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
lakini aliyezaliwa Burundi na kukulia Tanzania kabla ya kuhamia Sweden. Mhe.
Nyamko akitoa hotuba yake kwa Kiswahili alielezea namna kinavyoziunganisha nchi
hizi akisema hata anapokuwa nchini Kenya kibiashara hutumia pia lugha ya
Kiswahili.
Sherehe hizo zilifana
kwa wingi wa vyakula na vitu mbalimbali vinavyoitangaza Tanzania na utamaduni wa
Mswahili kama viungo, maonesho ya mitindo ya mavazi, sanaa za mapambo, ngoma,
nyimbo, mashairi na hadithi za watoto.
Shughuli hii ya
kipekee iliwakutanisha zaidi ya watu 500 ambao mbali ya Watanzania wengine
walikuwa ni raia au wenye asili za nchi za Afrika Mashariki na Kati, Waswidi
marafiki wa Tanzania na Mabalozi na wawakilishi wa nchi za Botswana, China, Eritrea, India,
Japan, Kenya, Misri, Nigeria, Rwanda na Zimbabwe.
Wadhamini walioshirikiana na Ubalozi ni benki mbili za nchini, NMB na CRDB; Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Kenzan Travel, Green Tours Tanzania na Monty's Glow.
Mgeni rasmi, Waziri wa zamani wa Masuala ya Usawa wa Jinsia wa Sweden, Mhe. Nyamko Sabuni, akihutubia kwa lugha ya Kiswahili katika maadhimisho hayo.
Maonesho ya sanaa na
mavazi ya utamaduni wa Kiswahili yaliyooneshwa jijini Stockholm tarehe 5 Julai,
2025, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani.
Maonesho ya sanaa na mavazi ya utamaduni wa Kiswahili yaliyooneshwa jijini Stockholm tarehe 5 Julai, 2025, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani.
0 Maoni