Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mej.Jen
(Mstaafu) Hamis Semfuko amesema kuna mwitikio mkubwa sana wa wananchi
kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii na takribani watalii zaidi ya
45,000 walitembelea banda hilo kwa siku ya jana Julai 5,2025.
Mej. Jen (Mstaafu)
Semfuko ameyasema hayo leo Julai 6,2025 alipotembelea Bustani ya Wanyamapori
katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya
Sabasaba akiambatana na Menejementi ya TAWA.
“Nimefurahi sana
kuona mwitikio mkubwa wa wananchi kutembelea banda la Wizara yetu hususan
katika Bustani ya Wanyamapori na hapa nimejulishwa kuwa kwa siku ya jana pekee
takribani wananchi 45,000 walitembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii,”
amesema Semfuko.
Mej. Jen (Mstaafu)
Semfuko ameongeza kuwa mwitikio huu wa wananchi umechagizwa na sababu
mbalimbali zikiwemo jitihada zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan katika kutangaza vivutio vya utalii
nchini.
“Tunamshukuru Mhe.
Rais kwa jitihada alizofanya za
kutangaza utalii zimesababisha watu wapende kuona wanyamapori na vivutio
vingine vya utalii,” ameongeza Semfuko.
Sambamba na hilo,
Semfuko amesema kuwa hivi karibuni TAWA imejipanga kuanzisha Bustani ya
Wanyamapori katika Visiwa vya Zanzibari katika Hifadhi ya Jambiani Muyuni.
“Hivi karibuni TAWA
tutapeleka mbawa zetu Zanzibar, ukifika Zanzibar, ukaenda Jambiani utatukuta
TAWA pale, hivyo karibuni sana,” amesema Semfuko.
Kwa upande wake,
Kaimu Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Mlage Kabange amesema TAWA imendelea kuleta
wanyamapori katika maonesho haya kwa lengo la kuwapa elimu wananchi kuhusu wanyamapori hao sambamba na
kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vya utalii.
Kadhalika, Kamishna
Kabange amesema wanashukuru kuona mwitikio mkubwa wa watu katika kuona
wanyamapori, Aidha, amesema kuwa baada ya maonesho ya Sabasaba kukamilika
wanyamapori hawa wataendelea kupatikana katika Hifadhi ya Pande iliyoko jijini
Dar es Salaam.
“Baada ya maonesho
haya kumalizika, wanyamapori hawa bado wataendelea kuwepo katika maeneo
mbalimbali tunayoyasimamia, kwa Dar es Salaam tuna eneo la Pande na wanyama
hawa wote waliopo hapa, wanapatikana kule hivyo tunawakaribisha wananchi baada
ya Sabasaba waendelee kutembelea maeneo tunayosimamia,” amesema Kamishna
Kabange.
Maonesho ya Sabasaba
bado yanaendelea katika viwanja vya Sabasaba hadi
ifikapo 13 Julai 2025.
Na. Joyce Ndunguru - Dar es Salaam
0 Maoni