Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeendelea kuthibitisha umahiri na uaminifu wake
katika operesheni za kimataifa baada ya Umoja wa Mataifa kupitia Ujumbe wa
Kulinda Amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA), kwa kulipatia jukumu
la ujenzi wa mradi muhimu wa madaraja katika Mkoa wa Mambere-Kadei.
Ujenzi wa madaraja hayo
matatu ni yale yaliyoharibika kwa muda mrefu, yakitatiza mawasiliano kati ya
vijiji na miji, na hivyo kuathiri upatikanaji wa huduma muhimu kama elimu,
afya, na masoko.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa mradi wa ujenzi huo, Katibu Mkuu wa Mkoa wa Equatorial, Mheshimiwa
Zouketchia Emmanuel, amelishukuru JWTZ kwa kujitolea kwao na mchango wao mkubwa
kwa wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
"Tumepata shida ya
usafiri kwa muda mrefu kwa sababu ya madaraja haya. Leo tunaona mabadiliko
yanayoletwa na MINUSCA kupitia marafiki
zetu wa kweli kutoka Tanzania. Asanteni sana JWTZ," alisema Katibu
Mkuu.
Naye Naibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa Mkoa wa Mambere-Kadei (ofisi ya MINUSCA, Berberati), Ndugu Landry
Muketchu, amesema kuwa Umoja wa Mataifa' umelipatia JWTZ kazi ya mradi unaotoa
matokeo ya haraka (Quick Impact Project) kwa kuwa limeendelea kuonesha nidhamu,
weledi na mshikamano wa hali ya juu katika kazi wanazofanya chini ya MINUSCA.
"Tumeamua kulipa
JWTZ ujenzi wa Madaraja haya kutokana na ukweli kwamba limekuwa likifanya kazi
zake kwa weledi wa hali ya juu kwa kila jukumu linalotolewa na Umoja wa
Mataifa' alisisitiza.
Naye Kamanda wa Kikosi
cha Nane cha Ulinzi wa Amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, (TANBAT 08)
Luteni Kanali Theophil Nguruwe, ameushukuru Umoja wa Mataifa' kupitia MINUSCA
kwa kuliamini JWTZ kwa kulipa jukumu hilo muhimu.
"Tunaahidi kutekeleza mradi huu kwa
weledi wa hali ya juu, kwa kuzingatia viwango vya Umoja wa Mataifa na
kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa," alisema Luteni Kanali
Nguruwe.
Wananchi waliohudhuria
hafla hiyo walionesha furaha zao na kutoa shukrani kubwa na kukiri kuwa mradi
huo ni hatua ya kweli ya kurejesha matumaini na ustawi katika maisha yao.
Mbali na mradi huu, JWTZ
limeendelea kulinda amani, kutoa misaada ya kibinadamu kama vile afya, ujenzi
wa shule pamoja na kushiriki michezo mbalimbali nchini humo.
MINUSCA ilianzishwa na
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2014 (kupitia azimio namba
2149) kwa lengo la kusaidia kurejesha utulivu, kulinda raia, kusaidia mchakato
wa kisiasa, kushughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu, na kusaidia ujenzi wa
Taasisi za Serikali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).
0 Maoni