Yajue mataifa 12 ambayo raia wake wamepigwa marufuku kuingia Marekani

 

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameidhinisha kuanza rasmi marufuku ya usafiri kwa raia wa mataifa 12 kuingia nchini humo, huku mataifa mengine saba yakikumbwa na vikwazo vya masharti ya kuingia Marekani.

Amri hiyo mpya ya utawala wa Trump, iliyosainiwa wiki iliyopita, imeanza kutekelezwa rasmi leo Jumatatu.

 Hatua hiyo inawalenga raia wa Afghanistan, Myanmar, Chad, Congo-Brazzaville, Guinea ya Ikweta, Eritrea, Haiti, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen, ambao sasa hawataruhusiwa kuingia Marekani.

Kwa upande mwingine, raia wa Burundi, Cuba, Laos, Sierra Leone, Togo, Turkmenistan na Venezuela watakabiliwa na masharti maalumu ya kusafiri, ikiwa ni pamoja na aina za viza zitakazotolewa na mazingira ya kiusalama.

Rais Trump amesema kuwa marufuku hiyo ni sehemu ya juhudi za kulinda usalama wa taifa lake dhidi ya vitisho vya kimataifa, na kwamba orodha hiyo inaweza kubadilika kulingana na hali ya kiusalama duniani.

“Iwapo kutakuwa na maendeleo makubwa kutoka mataifa haya, tuko tayari kufanya marekebisho. Lakini pia mataifa mengine yanaweza kuongezwa iwapo vitisho vipya vitaibuka,” alisema Trump katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Hatua hiyo imeibua wasiwasi kwa mashirika ya haki za binadamu na baadhi ya viongozi wa kimataifa, ambao wanahoji uhalali wa vigezo vilivyotumika na athari zake kwa familia, wahamiaji na wakimbizi waliokuwa wakitegemea usafiri kuelekea Marekani.

Chapisha Maoni

0 Maoni