Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amezitaka Ofisi ya Rais
– TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana kikamilifu katika kukamilisha mradi wa
ujenzi wa shule 56 za kuendeleza vipaji vya michezo.
Mhe. Majaliwa ametoa
agizo hilo leo, Juni 9, 2025, wakati wa ufunguzi rasmi wa mashindano ya Umoja
wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari
(UMISSETA), yaliyofanyika katika Viwanja vya Kichangani, Kata ya Kihesa,
Manispaa ya Iringa, mkoani Iringa.
Aidha, amezitaka
Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
kuhakikisha kuwa ratiba za michezo zinawekwa rasmi kwenye mipango ya kila shule
na kutekelezwa ipasavyo ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kushiriki michezo mara
kwa mara kwa lengo la kukuza vipaji.
"Katika shule zetu tunahitaji ratiba za
michezo ili vijana wetu baada ya masomo waweze kushiriki katika shughuli za
michezo. Hili litasaidia kuinua vipaji na kuwaandaa kwa mashindano haya ya
kitaifa," alisema Waziri Mkuu.
Mhe. Majaliwa
amevitaka vyama vya michezo vya kitaifa kupeleka wataalamu kwenye mashindano ya
UMITASHUMTA na UMISSETA ili kuwabaini wachezaji wenye vipaji maalum
watakaoendelezwa kwa lengo la kuunda timu bora za taifa.
Aidha, amewaagiza
Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuhakikisha walimu wa michezo wanapewa mafunzo
maalum ya kisasa kuhusu sheria, mbinu na mabadiliko ya michezo, na kuwapeleka
kwenye vyuo vya michezo vilivyopo nchini ili kuongeza ufanisi wa ufundishaji.
Waziri Mkuu pia ameagiza
Kituo cha Mafunzo cha Malia kutumika kikamilifu kwa ajili ya kuwajengea uwezo
walimu wa michezo ili kusaidia kukuza vipaji vya wanafunzi katika ngazi ya
shule.
Vilevile, amezitaka
Halmashauri zote nchini kuhakikisha maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa michezo
hayavamiwi na shule zote za msingi na sekondari zinakuwa na viwanja kwa ajili
ya michezo mbalimbali inayoshirikishwa kwenye mashindano haya.
Ameitaka TAMISEMI,
kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuandaa mpango
mkakati wa kitaifa utakaohakikisha kila shule inakuwa na miundombinu ya
michezo, ikiwemo viwanja vya riadha, ili kuimarisha ushiriki wa wanafunzi
katika michezo.
Pia, amezihimiza
taasisi hizo kushirikiana na wadau wa michezo, kama makampuni ya biashara
yanayodhamini michezo, kuendeleza vipaji vilivyoibuliwa mashuleni kwa lengo la
kuzalisha wanamichezo bora.
Kwa upande mwingine,
Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoa vibali kwa
shule binafsi na academies zinazolenga kukuza vipaji vya michezo kuanzia ngazi
ya awali, ili ifikapo umri wa miaka 14 vijana wawe wameimarika kitaaluma na
kimwili.
Mwisho, amewataka
Watanzania wote kujenga tabia ya kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara ili
kuwa na afya bora ambayo ndio msingi wa
taifa lenye nguvu.
Na. OR-TAMISEMI -
Iringa
0 Maoni