Mtendaji Mkuu wa
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff
amewataka makandarasi wanaotekeleza kazi za ukarabati na matengenezo ya
barabara vivuko na madaraja katika
maeneo yaliyoharibiwa na mvua za El nino nchini kutekeleza mikataba yao kwa
wakati huku wakizingatia masuala ya msingi ikiwemo usalama mahali pa kazi
pamoja na utunzaji wa mazingira.
Mhandisi Seff
ameyasema hayo wakati wa kikao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam kati ya
TARURA na Makandarasi hao wanaotekeleza miradi hiyo nchi nzima.
“Hakikisheni katika
utekelezaji wa miradi yote mnakamilisha kwa wakati pia mnazingatia masuala yote
ya usalama na mazingira kama ilivyoainishwa kwenye makubaliano ya jumla ya
miradi hii,” alisisitiza.
Naye, Mratibu wa
miradi ya Benki ya Dunia kutoka TARURA Mhandisi Humphrey Kanyenye amesema
kwamba wao kama waratibu wa miradi hiyo wapo tayari kuhakikisha wanatoa
ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kila mkandarasi anatekeleza majukumu yake
kwa ufanisi ikiwemo utunzaji wa mazingira ili kuepuka kwenda kinyume na matakwa
ya utekelezaji wa miradi ya benki ya dunia.
Wakati huohuo Meneja
wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga amewahakikishia
ushirikiano makandarasi kuhakikisha wanakimbizana na muda na kukamilisha miradi
hiyo yenye tija kwa mkoa wake pamoja na nchi nzima kwa wakati kwani Dar es
Salaam ni moja ya mkoa wenye miradi hiyo ya dharura.
Aidha, katika kikao
hicho makandarasi walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali kwa uelewa
zaidi kabla ya kuanza utekelezaji wa kazi ambapo walijibiwa na kuhakikishiwa
kuwa TARURA kwa niaba ya Katibu Mkuu OR TAMISEMI itahakikisha hakuna mkwamo
wowote kwani dhamira ya Serikali ni kuona miradi inakamilika kwa wakati kama
ilivyopangwa.
Miradi ya SERC
inatekelezwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa DMDP II ambapo
mtekelezaji mkuu ni Katibu Mkuu OR-TAMISEMI ambapo amekasimu utekelezaji huo
kwa Mtendaji Mkuu TARURA.
0 Maoni