Zaidi ya shilingi
Bilioni 2.4 zimetengwa na Serikali kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa mwaka
2025 kwa ajili ya Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi
na Sekondari.
Hayo yameelezwa na
Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Mhe. Zainab Katimba
wakati wa uzinduzi wa Mashindano hayo kitaifa katika viwanja vya Kichangani
kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa Mkoani Iringa.
"Nitumie nafasi
hii kumshukuru sana Mhe.Rais kwa kuendelea kutuwezesha na kutupatia fedha za
kutosha kuandaa na kuendesha mashindano haya kila mwaka, jambo ambalo
limeendelea kukuza sekta ya michezo Nchini," amesema Mhe. Katimba na
kuongeza,
"Michezo ya
UMITASHUMTA na UMISSETA imekuwa na mchango mkubwa katika kuandaa wanamichezo wa
timu za Taifa ambao wamekuwa wakiliwakilisha Taifa katika michezo mbalimbali."
Aidha, Mhe.Katimba
amesema kuwa michezo ya shule imekuwa sehemu ya kuimarisha Muungano kutokana na
ushiriki wa wanafunzi kutoka Tanzani Bara na Visiwani Zanzibar.
Mashindano ya
UMITASHUMTA na UMISSETA inafanyika Mkoani Iringa, ikiwa ni zaidi ya miaka 30
tangu yalipofanyika kwa mara ya mwisho Mkoani humo.
Na. OR-TAMISEMI


0 Maoni