Wakala wa Vipimo
(WMA) umetekeleza Mpango Kazi wake wa Mwaka wa Fedha 2024/2025 kwa asilimia 96
ya malengo iliyojiwekea, kufikia mwezi Mei mwaka huu.
Hayo yalibainishwa
Juni 13, 2025 na Mtaalamu wa Uchumi kutoka Kitengo cha Mipango cha WMA,
Benjamin Nkwera wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti
kwa kipindi husika kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi lililoketi katika
Ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Katika taarifa yake,
Mtaalamu huyo wa Uchumi alieleza kwamba katika kipindi husika, mikoa 25
imefanikiwa kufikia malengo kwa asilimia 100 huku mikoa minne ikifikia malengo
kwa zaidi ya asilimia 90 na miwili ikiwa na asilimia chini ya 80.
Miongoni mwa kazi
zilizotekelezwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa Makao Makuu ya Wakala jijini
Dodoma, ununuzi wa magari na vitendea kazi vingine, pamoja na kuajiri wataalamu
katika kada mbalimbali.
Aidha, alieleza kuwa
Wakala imefanikiwa kuhakiki vipimo 1,191,833 kati ya 1,238,391 sawa na asilimia
96.24 ya lengo.
“Kati ya vipimo
vilivyokaguliwa na kuhakikiwa, vipimo 16,210 vilirekebishwa na 1,161
vilikataliwa,” alidadavua Nkwera.
Aliongeza kuwa katika
kipindi husika, Wakala imefanya kaguzi 4,231 kati ya 3,667 zilizopangwa, sawa
na asilimia 115.38.
Kazi nyingine
iliyotekelezwa ni ukaguzi na ufuatiliaji wa vipimo vinavyotumika kwenye
ushushaji wa mafuta jamii ya petroli pamoja na mafuta ya kula ambapo alisema
kuwa jumla ya Meli 161 zilizoingia nchini zenye jumla ya lita 9,955,936,919
zilikaguliwa.
Akizungumza na
wajumbe wa Baraza hilo, Mwenyekiti wake ambaye ni Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban
Kihulla aliwaasa kufanya kazi kwa bidii, upendo na kushikamana huku
wakijiepusha na vitendo vya rushwa ili kuendelea kupata matokeo chanya kwa
faida ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Naye Mwakilishi wa
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE), Mkoa wa Dar es Salaam,
Sara Rwezaula alipongeza ushirikiano uliopo baina ya Uongozi wa Wakala na
wafanyakazi ambao alisema ndiyo hasa ulioleta chachu ya matokeo chanya ya
utendaji wa WMA.
“Nampongeza na
kumshukuru Mtendaji Mkuu na Menejimenti yote kwa kuendelea kutekeleza maelekezo
yanayotolewa na Baraza la Wafanyakazi,” alisisitiza.
Kikao hicho cha 36
cha Baraza la Wafanyakazi la Wakala wa Vipimo kilitanguliwa na kikao cha Kamati
Tendaji kilichofanyika siku moja kabla, Juni 12, 2025.
Wakala wa Vipimo ni
moja ya Wakala na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Jukumu
lake kuu ni kumlinda mlaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kupitia matumizi ya
vipimo sahihi na kwa usahihi.
0 Maoni