WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa amesema kuwa katika mwaka 2025/2026 Serikali imepanga kutoa mikopo kwa
wanafunzi 252,773 wakiwemo 88,320 wa mwaka wa kwanza ili kuwafikia wanafunzi
wengi zaidi.
Mhe. Majaliwa amesema hayo leo Jumamosi (Juni 14, 2025)
wakati wa maadhimisho ya miaka 21 ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu
ya Juu, yanayofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
“Huu ni muendelezo wa malengo ya Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha elimu ya juu na mazingira
ya wanafunzi kwa ujumla, Mwaka 2024/2025, mikopo ya shilingi bilioni 787.4
imetolewa kwa wanafunzi 248,331 ikilinganishwa na bilioni 570 kwa wanafunzi
177,925 mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 40”.
Kwa upande wa Ufadhili wa Samia (Samia
Scholaship) Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026
wanafunzi 2,630 watapatiwa Ufadhili wa kupitia progamu hiyo ambayo mpaka sasa
jumla ya wanafunzi 1,976 wananufaika na ufadhili huo . “Programu hii ni kwa
ajili ya wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha Sita katika
masomo ya Sayansi”.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema ili
kuleta unafuu katika urejeshaji wa mikopo, Serikali imeondoa adhabu na tozo ya
kulinda thamani katika urejeshaji wa mikopo kwa lengo la kuongeza unafuu kwa
wahitimu. “Hatua hii imeongeza marejesho ya mikopo. Vilevile, imetengenezwa
Mfumo wa Marejesho unaotumika na taasisi 3,565, na mfumo wa utambuzi unaotumika
na wanufaika takriban 3,000 kwa mwezi.”
Akizungumzia kuhusu
kuanzishwa kwa utaratibu wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa Stashahada,
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika mwaka 2023/2024 mpango huo ulianza kwa
kutoa mikopo ya shilingi bilioni 7.29 na mwaka 2024/2025 ziliongezwa hadi
kufikia shilingi bilioni 19.95 sawa na ongezeko la asilimia 177.6.
“Mpango huu
unahusisha fani za kipaumbele ambapo jumla ya wanafunzi 13,214 wamenufaika hadi
sasa”
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanavyuo wote nchini kutokubali kutumika
na baadhi ya wanasiasa wenye nia ovu ya kuwavuruga na kilifanya Taifa liishi
bila amani “Tanzania ni yetu, endeleeni kuhakikisha kuwa Taifa hili linabaki
salama pamoja na uchaguzi tulionao mbele yetu.”
Kadhalika ametoa wito
kwa viongozi wa Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO)
kuhakikisha wanahimizana kuwa mfano mzuri kwa jamii. “Tambueni kuwa Taifa zima
linawaangalia ninyi kama kioo cha jamii, jiepusheni na vitendo vilivyo kinyume
na maadili ya Kitanzania ikiwemo ushoga, usagaji, na matumizi ya madawa ya
kulevya.”
Naye, Naibu Waziri
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Qs Omar Kipanga amesema Wizara
hiyo inaendelea na mpango wa kusimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo
ya Mwaka 2014 toleo la 2023 yenye kulenga kutoa elimu inayozingatia ujuzi
kulingana na mahitaji ya soko la ajira na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
“Katika kufanikisha
utekelezaji wake, tumefanikiwa kuhuisha mitaala na kuandaa miongozi mbalimbali
yenye lengo la kuhakikisha elimu inayotolewa nchini inazingatia viwango vya
kitaifa, kimataifa na kuwajengea wahitimu ujuzi unaohitajika katika karne ya
21.”
Kwa Upande wake Rais
wa Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) Geofrey Kiliba amesema
kuwa taasisi hiyo inaishukuru Serikali kwa maboresho makubwa katika sekta ya
elimu ya juu, Elimu ya Mafunzo na Ufundi Stadi kuanzia miundombinu, kuongezeka
kwa bajeti ya mikopo, kuimarisha kwa mitaala na usimamizi bora wa vyuo na
taasisi za elimu ya juu.
“Sisi TAHLISO tupo
tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika nyanja zote ikiwemo kisera na
kielimu ili kuchochea maendeleo makubwa zaidi kwa Taifa letu.”
0 Maoni