Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewaasa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Bukombe wasikubali kuvutana na kugombana bali wadumishe amani, kuendelea kuheshimiana na kulinda utu wao hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Dkt. Biteko amesema
hayo Juni 14, 2025 wilayani Bukombe, mkoani Geita mara baada ya kuzindua maduka
31 ya kisasa yaliyopo katika eneo la Ofisi za CCM wilayani humo.
“Naomba niwakumbushe
tena kwa sasa tunaukaribia mwezi wa Oktoba, 2025. Tunakaribia kuingia katika
zoezi la Uchanguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, niwaombe tu kwamba, zoezi la
uchaguzi ni zoezi la mara moja, lakini maisha yetu sisi yanadumu na yataendelea
kudumu na kuna maisha baada ya kampeni na baada ya Uchanguzi. Hivyo, kwa
heshima, nawaomba tuendelee kudumisha umoja, upendo na undugu uliopo baina
yetu,” amesema Dkt. Biteko.
Katika hatua
nyingine, amezungumzia ujenzi wa maduka hayo ya kisasa kuwa ni hatua kubwa kwa
maendeleo ya wananchi wa eneo hilo la Ushirombo na maeneo mengine ya jirani kwa
kuwa ni chanzo cha maendeleo na mzunguko wa fedha katika eneo hilo.
Amesisitiza “ Maduka
haya yataongeza mvuto na hivyo kuongeza thamani ya eneo hili la ardhi pamoja na
thamani ya jengo. Ukuaji wa eneo letu hili huchangiwa zaidi na shughuli za
madini na shughuli nyingine za kiuchumi. Taarifa zinaonesha kuwa, Mkoa wa Geita
umeonesha kasi kubwa zaidi ya ukuaji kutokana na shughuli za madini, na watu
wanaochimba watapata huduma kwenye hili.”
Aidha, amewapongeza
na kuwashukuru Mwenyekiti na Katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe na Madiwani 23 kwa
ushirikiano wao na kusema kuwa wamefanya kazi kubwa ya kuchangia ujenzi wa
maduka hayo na kusema kuwa anafurahishwa kufanya kazi nao akiongeza kuwa
wajumbe wa kata wanazotoka wanaweza kuwapima kwa kazi walizofanya.
Dkt. Biteko amesema
kuwa CCM katika wilaya hiyo itaendelea kuunga mkono mawazo mapya yatakayotolewa
kwa ajili ya kusaidia maendeleo ambapo ametaja baadhi ya miradi ya ujenzi wa
soko, stendi na barabara inayoendelea kujengwa wilayani humo inalenga kukuza
uchumi wa wilaya na mkoa kwa ujumla.
Vilevile, Dkt. Biteko
awaomba wanachama wa CCM kumuunga mkono kwa kumchagua Rais Samia na mgombea
mwenza Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba
mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Geita, Nicholous Kasendamila amewapongeza CCM Wilaya ya Bukombe kwa ujenzi
wa maduka hayo na kusema kuwa hilo ni darasa na siasa ni uchumi na ni wajibu wa
CCM kukiimarisha chama chao.
Naye, Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Mkoa wa Geita, Evarist Gervas
amepongeza Dkt. Biteko kwa kuimarisha Chama katika wilaya hiyo na kushirikiana vizuri na viongozi wa
Chama kwa kuimarisha wilaya hiyo kiuchumi.
Awali akitoa taarifa
ya ujenzi wa maduka hayo ya kisasa, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya
Bukombe, Leonard Mwakalukwa amesema kuwa Wilaya hiyo inatimiza sera ya CCM ya miradi ya uwekezaji
na kwa kutambua kauli mbiu ya siasa na uchumi, ilitekeleza wazo la ujenzi wa maboresho
ya vibanda hivyo 21 vilivyokuwepo awali liliasisiwa na Mbunge wa jimbo la
Bukombe Dkt. Biteko.
Amesema Dkt. Biteko
alitoa wito wa kuwa na vitega uchumi zaidi vya Chama cha Mapinduzi na kutunza
na kuboresha mandhari ya eneo la CCM la Wilaya ya Bukombe. Ndipo Halmashauri
Kuu ya CCM Wilaya ya Bukombe ikapitisha pendekezo hilo.
Ametaja faida za
mradi kuwa ni pamoja na CCM wilayani humo kukusanya mapato kwa wingi.
0 Maoni