Hifadhi ya Taifa ya
Mpanga/Kipengere, inayopatikana katika mikoa ya Mbeya na Njombe, inajiandaa
kuandika historia mpya kwa kuadhimisha Siku ya Maporomoko Duniani kwa kishindo
kikubwa, Juni 16 mwaka huu.
Katika maadhimisho
hayo, kutakuwa na Nyamapori Festival, sambamba watu kufurahia ladha halisi ya
vyakula vya asili vitakavyoandaliwa kwa kuzingatia mila na tamaduni za wakazi
wa maeneo yanayozunguka hifadhi hiyo.
Miongoni mwa mambo
makubwa yatakayofanyika siku hiyo ni uzinduzi rasmi wa barabara inayowawezesha watalii kufika kwa urahisi
katika eneo la kipekee la bustani ya dunia, eneo ambalo awali lilikuwa na changamoto ya
miundombinu, sasa limefunguliwa rasmi kwa mara ya kwanza.
Kwa mujibu wa taarifa
kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), barabara hiyo sasa
imekamilika na inawawezesha watalii kufika katika eneo hilo lenye kapeti la
maua ya aina mbalimbali, tukio ambalo
litakuwa la kwanza kabisa kushuhudiwa na wageni wa ndani na nje ya nchi.
"Hii ni fursa
adimu ya kushuhudia mandhari ya kuvutia, yakiwemo maporomoko 58 ya maji ndani
ya hifadhi, pamoja na vivutio vingine vingi vya kiasili," imesema sehemu
ya taarifa ya TAWA.
Wakazi wa maeneo ya
karibu, wageni kutoka sehemu mbalimbali nchini, na hata wageni wa kimataifa,
wanahimizwa kujitokeza kushiriki katika tukio hili la kihistoria litakalotoa
taswira halisi ya utalii wa ndani unaozingatia mazingira, utamaduni, na
uhifadhi endelevu.

0 Maoni