Wawili washikiliwa kwa kutaka kumuua mama yao

 

Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kupanga njama ya kumuua mama yao mzazi kwa imani za kishirikina, katika tukio ambalo pia mtoto mwenye umri wa miaka minne alijeruhiwa kwa risasi. Aidha, mtuhumiwa mmoja wa tukio hilo ameuawa kwa kupigwa risasi wakati wa mapambano na polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamini Kuzaga, amesema tukio hilo lilitokea usiku wa Juni 13, 2025, majira ya saa 6:05 katika Kijiji cha Ipwizi, Kata ya Mjele, Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Kamanda Kuzaga alieleza kuwa katika tukio hilo, mtoto aitwaye Sinzo Jifwalo (4), alijeruhiwa kwa risasi za shotgun begani na mdomoni akiwa amelala ndani ya chumba pamoja na bibi yake, Bi. Kweji Lugembe (75), ambaye ndiye alilengwa kuuawa.

Taarifa za awali zinaonesha kuwa tukio hili linahusishwa na imani za kishirikina ambapo watoto wa Bi. Kweji waliwahi kumtuhumu mama yao kuwa anajihusisha na ushirikina unaodaiwa kusababisha vifo vya baadhi ya watoto wa familia hiyo,” alisema Kamanda Kuzaga.

Watuhumiwa wakuu wa tukio hilo ni Seven Kipara (38) na mdogo wake Jifaru Kipara, ambao wanadaiwa kupanga njama ya mauaji kwa kumkodi mtu anayejulikana kwa jina la Tabi Deus (39), mkazi wa Kilwa Masoko – Lindi, kwa makubaliano ya kumlipa shilingi milioni tano. Tabi Deus aliandamana na mshirika wake anayefahamika kwa jina la Shija.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, mnamo Juni 8, Tabi Deus na Shija walifika Mji Mdogo wa Mbalizi ambako walipokelewa na Seven Kipara na kisha kufikishwa katika eneo la tukio. Juni 13 usiku, Deus alifyatua risasi mbili kupitia dirishani akiwa na lengo la kumuua Bi. Kweji, lakini risasi hizo zilimpata mtoto mdogo aliyejeruhiwa vibaya.

Polisi walifanikiwa kuwakamata Tabi Deus na Seven Kipara, ambapo Deus alikutwa na bastola ya kutengenezwa kienyeji isiyo na namba pamoja na risasi mbili za shotgun ndani ya mkoba.

Mnamo Juni 15, saa 1:00 jioni, Tabi Deus aliwaongoza polisi hadi maficho ya mshirika wake Shija pamoja na silaha. Hata hivyo, Shija alipoona askari, alijaribu kukimbia na kuwapuuza walipomwamuru asimame. Polisi walifyatua risasi tatu hewani, lakini Shija aliendelea kukimbia ndipo alipolengwa na kupigwa risasi mguuni. Alikimbizwa katika Hospitali Teule ya Ifisi ambako alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.

Kamanda Kuzaga amesema kuwa msako wa kuwatafuta watuhumiwa wengine unaendelea, na ametumia nafasi hiyo kuwaonya wote wanaojihusisha na vitendo vya kishirikina na mauaji kuwa sheria haitasita kuchukua mkondo wake.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako wa watuhumiwa waliobakia na tunatoa onyo kali kwa yeyote anayehusika na vitendo vya kishirikina – sheria itachukua mkondo wake bila muhali,” amesema Kamanda.

Jeshi la Polisi pia limewaasa wananchi kuachana na imani potofu na kutafuta suluhisho la migogoro kupitia njia za kisheria badala ya kujichukulia sheria mikononi.


Chapisha Maoni

0 Maoni