Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George
Simbachawene ameipongeza Tume ya Madini kwa kazi kubwa na yenye matokeo chanya
katika ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuchochea maendeleo ya Sekta ya
Madini nchini.
Akizungumza
alipotembelea banda la Tume ya Madini katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa
Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Mhe.
Simbachawene amesema mafanikio hayo ni matokeo ya uongozi thabiti wa Waziri wa
Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde.
“Nawapongeza Tume ya
Madini, na nampongeza sana Waziri wenu Mheshimiwa Anthony Mavunde kwa kusimamia
kwa weledi ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kufufua migodi iliyokuwa
imesimama, pamoja na kutoa ajira kwa vijana. Haya ni mafanikio ya kujivunia,”
amesema Mhe. Simbachawene.
Ameeleza kuwa Sekta
ya Madini kwa sasa inachangia zaidi ya asilimia 10 ya Pato la Taifa, jambo
linaloonesha mchango mkubwa wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa, huku akitoa
wito kwa Tume ya Madini kuongeza juhudi zaidi ili kuvuka lengo la sasa.
Katika hatua
nyingine, Waziri Simbachawene amesema kaulimbiu ya Sekta ya Madini inayosema
“Madini ni Maisha na Utajiri” siyo kauli ya bahati nasibu, bali ni uthibitisho
wa mchango wa sekta hiyo katika kuimarisha maisha ya Watanzania na kuongeza
utajiri wa Taifa.
“Hii si kauli ya
bahati mbaya. Sekta hii ina mchango wa kweli katika nyanja zote, ajira,
biashara, teknolojia, na mapato ya ndani. Tume ya Madini ifanye kazi kwa nguvu
zaidi ili Watanzania wote wanufaike na rasilimali zao,” ameongeza.
Maonesho ya Wiki ya
Utumishi wa Umma mwaka huu yamejumuisha taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo
za sekta ya madini, zikionesha mafanikio, huduma, na mipango ya maendeleo kwa
wananchi. Banda la Tume ya Madini limeendelea kuvutia wananchi wengi wanaotaka
kupata elimu kuhusu fursa zilizopo kwenye sekta ya madini, hususan kwa
wachimbaji wadogo na wajasiriamali wa ndani.
0 Maoni