Mwanafunzi wa MUST ashikiliwa kwa mauaji ya mwenzake

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Emilian Joseph Duzu (21) kwa tuhuma za kumuua kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali mwanafunzi mwenzake wa mwaka wa tatu, Gerald Philbert Said (22).

Tukio hilo lilitokea alfajiri ya Juni 14, 2025, majira ya saa 11:00, katika klabu moja inayojulikana kama Mbeya Pazuri, iliyopo Jijini Mbeya.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamini Kuzaga, amesema kuwa mtuhumiwa Emilian Duzu anadaiwa kumchoma marehemu Gerald Philbert Said tumboni kwa kutumia kitu chenye ncha kali, hali iliyosababisha majeraha makubwa.

“Baada ya tukio hilo, marehemu alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa matibabu, lakini alifariki dunia majira ya saa 7:00 mchana siku hiyo hiyo,” alisema SACP Kuzaga.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliosababishwa na ulevi wa kupindukia. Inadaiwa kuwa wawili hao walikuwa wakibishana ndani ya klabu hiyo, na walinzi (mabaunsa) waliamuru watoke nje. Hapo ndipo mtuhumiwa alielekea kwenye gari lake alikokuwa ameegesha nje, na marehemu alimfuata kwa lengo la kuendeleza ugomvi huo, ndipo akachomwa na kitu chenye ncha kali.

Kamanda Kuzaga ametoa wito kwa wananchi, hususan vijana na wanafunzi wa vyuo vikuu, kuzingatia maadili, kujiepusha na ulevi wa kupindukia na kutatua tofauti zao kwa njia ya amani.

“Vitendo vya uhalifu havina nafasi katika jamii. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya litaendelea kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo vya namna hii,” amesisitiza Kamanda Kuzaga.

Mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria, huku uchunguzi ukiendelea.

Chapisha Maoni

0 Maoni