Maelfu ya wananchi
kutoka Mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani wamejitokeza kwa wingi katika viwanja
vya Chinangali kushiriki Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, huku wengi
wakivutiwa na Banda la Tume ya Madini ambalo limekuwa kitovu cha elimu na maarifa
kuhusu Sekta ya Madini.
Banda hilo limekuwa
kivutio kikubwa kutokana na utoaji wa elimu ya kina kuhusu aina mbalimbali za
madini yanayopatikana nchini, taratibu za
upatikanaji wa leseni za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya
madini pamoja na fursa za kiuchumi zinazopatikana kupitia sekta hiyo.
Wananchi wa rika zote
wameonekana kuwa na shauku kubwa ya kupata uelewa kuhusu namna bora ya
kushiriki kwenye shughuli za madini kwa njia salama, endelevu na zenye tija
kwao binafsi na kwa taifa.
Afisa kutoka
Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na
Mazingira kutoka Tume ya Madini, Ashen
Mwambage ametoa elimu kwa wananchi kwa
umahiri mkubwa, akielezea kwa kina umuhimu wa kulinda mazingira wakati wa
shughuli za madini na namna ya kuzingatia sheria na taratibu ili kunufaika
ipasavyo.
“Tunahamasisha
wananchi kutumia fursa zilizopo katika Sekta ya Madini kwa kuzingatia kanuni za
usalama na utunzaji wa mazingira. Sekta hii ni mhimili muhimu wa uchumi wetu,
na kila Mtanzania ana nafasi ya kunufaika nayo,” ameeleza Mwambage.
Aidha, wananchi
wamepongeza juhudi za Tume ya Madini kwa kupeleka huduma karibu na wananchi
kupitia maonesho hayo, wakisema elimu waliyoipata itawawezesha kufanya maamuzi
sahihi kuhusu ushiriki wao katika sekta ya madini.
Tume ya Madini itaendelea
kutoa elimu kwa wananchi katika kipindi chote cha maadhimisho, huku ikisisitiza
ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya sekta hiyo yenye mchango mkubwa katika
Pato la Taifa.
Kaulimbiu ya
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa Mwaka huu inayotarajiwa kumalizika Juni 23, 2025 ni “Himiza
Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na
Kuchagiza Uwajibikaji.”



0 Maoni