Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) linatarajia kuanza kugawa nyumba za makazi 560 kwa wanunuzi wa
nyumba za mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) uliopo Kawe Jijini Dar es Salaam baada ya kukamilika kwa mradi
huo.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC
Hamad Abdallah Hamad amesema katika wiki ya mwisho ya mwezi huu wa Juni, 2025
wataanza kuwagawia wamiliki nyumba 200 zilizokwisha kamilika kati ya nyumba 560
za Samia Housing Scheme Kawe.
“Wiki ya mwisho ya
mwezi huu (Juni) tutaanza kuwagawia wamiliki wa Samia Housing Scheme nyumba 200
na hadi kufikia katikati ya Julai tutakuwa tumewakabidhi wamiliki wote nyumba
zao katika mradi wa Samia Housing Scheme Kawe awamu ya kwanza,” amesema Bw.
Hamad.
Amesema nyumba hizo 560
za Samia Housing Scheme za majengo kumi ya ghorofa yenye ghorofa kumi kila moja
zilizojengwa katika eneo la Kawe Jijini Dar es Salaam na kuuzwa zote zimejengwa
gharama ya Shilingi bilioni 48.
Bw. Hamad ambaye
alikuwa akiongea na wahariri wa vyombo vya habari jana Jijini Dar es Salaam
amesema NHC linaendelea na mapango wa ujenzi wa nyumba 5,000 za gharama ya kati
chini kupitia mradi wa Samia Housing Scheme ambao utekelezaji wake unaendelea.
Amesema mradi huu wa
nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo
kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya ujenzi wa nyumba bora nchini.
Bw. Hamad amesema Shirika
la Nyumba ya Taifa litaendelea na ujenzi wa nyumba 5,000 za Samia Housing
Scheme katika maeneo mbalimbali nchini ambayo ameyataja kuwa ni ya Medeli,
Mtoni Kijichi, Kawe 711 na Iyumbu.
Ameeleza kuwa asilimia
50 ya nyumba hizo zitajengwa katika Mkoa wa Dar es Salaam, asilimia 20 katika
mkoa wa Dodoma na asilimia 30 zitajengwa katika mikoa mingine.
Aidha, Bw. Hamad
amesema mradi huu wa nyumba 5,000 unaotekelezwa kwa awamu, utagharimu takriban Shilingi
bilioni 466 sawa na dola za Kimarekani milioni 200.
Ameeleza kuwa awamu
ya pili ya utekelezaji wa mradi huu imeanza eneo la Medeli, Jijini Dodoma; na
Kawe na Kijichi Jijini Dar es Salaam ambapo nyumba 908 zinajengwa. Ujenzi wa
nyumba 68 Iyumbu zimekamilika kwa asilimia 100.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika
la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah Hamad akizungumza na wahariri wa vyombo
vya habari Jijini Dar es Salaam.

0 Maoni