VITA YA IRAN: Bei ya mafuta duniani yatarajiwa kupanda

 

Bei ya mafuta duniani zinatarajiwa kupanda pale masoko ya nishati yatakapoanza kufanya biashara siku ya Jumatatu asubuhi huko Asia, kufuatia shambulio la Marekani dhidi ya Iran.

Taarifa kutoka katika masoko ya kimataifa zinaonyesha kuwa bei ya mafuta aina ya Brent ilifunga wiki ya biashara siku ya Ijumaa kwa dola 77.01 kwa pipa, ikiwa ni ongezeko la karibu asilimia 20 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Hata hivyo, wataalamu wa masoko wanasema kuwa pamoja na ongezeko hilo la bei, bado kiwango hicho kiko chini ya bei zilizoshuhudiwa katika kipindi kama hiki mwaka uliopita.

Gharama ya mafuta ghafi huathiri mambo mengi, kuanzia kiasi cha pesa unachohitaji kujaza gari lako mafuta hadi bei ya vyakula kwenye maduka makubwa ya rejareja.

Ongezeko la bei ya mafuta ghafi lina madhara makubwa kwa uchumi wa kila siku, hasa kwa nchi zinazoagiza mafuta kutoka nje, kama Tanzania.

Mabadiliko ya bei ya mafuta huathiri moja kwa moja gharama za usafirishaji, uzalishaji viwandani, na bei za bidhaa muhimu kama vyakula, mbolea na huduma nyinginezo.

Kwa takwimu za 2023 Iran ilikuwa nchi ya 7 kwa ukuzaji wa mafuta ghafi duniani ikiwa na uzalishaji wa takriban mapipa 3.94 milioni ya mafuta kwa siku.

Chapisha Maoni

0 Maoni