Taasisi ya Wanahabari
ya kusaidia jamii za Asili (MAIPAC) imezindua mpango wa ugawaji bure majiko ya
gesi kwa jamii za Asili ili ziweze kutumia nishati safi na salama ya Kupikia na
kupunguza matumizi ya kuni.
Mpango huo
uliozunduliwa kijiji cha Mbuyuni kata ya Makuyuni wilayani Monduli jana unalenga kugawa Majiko 1000 ikiwa ni jitihada
za shirika hili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama lakini pia
kuunga mkono kampeni ya Rais Samia
Suluhu kuhamasisha matumizi ya nishati safi na Salama nchini.
Akizungumza katika
hafla ya uzinduzi wa Tasisi ya Smile Youth and Women Support Organization
(SYWSO) na kugawa majiko hayo, kijiji cha Mbuyuni wilayani Monduli, Mbunge wa
Monduli Fred Lowassa alipongeza MAIPAC na SYWSO kwa kuamua kusaidia jamii.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na mamia ya
watu licha ya MAIPAC kutoa majiko, SYWSO
na MATT Fondation walikabidhi baiskeli za wenye ulemavu, fimbo za
kutembelea na vifaa vya shule.
Lowassa alisema moyo wa
kusaidia jamii ambao umeoneshwa na mashirika hayo unafaa kuigwa na wakazi wa
Monduli na Watanzania kwa ujumla kwani pia aliyekuwa Mkurugenzi wa IPP Hayati
Reginald Mengi alikuwa akifanya hjvyo.
Alisema amepata
faraja sana kuona wanahabari wameanzisha taasisi za kusaidia jamii na kuanza na
wilaya ya Monduli.
"Mimi binafsi
leo nimepata faraja sana kumuona hapa rafiki yangu mwandishi wa habari
mahiri Mussa Juma kwani siku nyingi tangu nikiwa kijana mdogo
nakumbuka kila siku asubuhi tulikuwa tunasubiri kusoma gazeti la _mwananchi_
kujua Mussa Juma ameandika nini,” alisema.
Alisema
sasa licha ya kuendelea na kazi ya kutupa habari lakini Juma na wenzake
wameamua kuanzisha taasisi za kusaidia jamii nawapongeza sana.
Alisema wananchi wa
Monduli wamepata faraja kupokea misaada hiyo kwani ni mwendelezo wa misaada kwa
Jamii.
Alisema Rais Samia
Suluhu pia amefanya makubwa katika wilaya hiyo ikiwepo kuleta mradi mkubwa wa
maji wa bilioni 27 ambao utasaidia Kata
ya Nanja na vijiji 13 vikiwepo vya kata ya lepurko vya Mbuyuni, Makuyuni na
Losimongori.
Alisema pia kilomita
3 za barabara katika kijiji hicho zimeanza kukarabatiwa na kutatua shida ya
barabara.
"Lakini pia kutokana na jitihada zangu
kama Mbunge niliweza kuonana na Rais Samia kuzungumzia mgogoro wa ardhi ya
malisho uliokuwepo hapa Monduli na sasa ametoa uamuzi ardhi hiyo tutatumia kwa
pamoja na jeshi letu la wananchi kwa malisho.”
"Nawaomba Monduli mwezi Octoba tumpe
kura zote Rais Samia kwani ametufanyia mambo makubwa na mengi ikiwepo kutoa
fedha sekta za afya, elimu na kusaidia wafugaji," alisema.
Juma alimshukuru
Lowassa kuhudhuria hafla hiyo na kugawa misaada hiyo ambayo inatokana na
michango ya taasisi na makampuni ya ndani nchini.
"Mheshimiwa
Mbunge misaada hii inatokana ma michango ya Taasisi za kitanzania na ambazo
zimeona umuhimu wa kusaidia jamii badala ya kutegemea mashirika kutoka nje ya
nchi na sisi MAIPAC tunaomba wadau waendelee kujitokeza kuchangia majiko
ili yasambazwe kwenye jamii hizi za
asili,” alisema.
Alisema Taasisi ya MAIPAC imekuwa na miradi kadhaa wilaya za Longido,
Karatu na Monduli ikiwepo Mradi wa
ujenzi wa uzio chanzo cha maji cha Kabambe kijiji cha Selela ambao
umekamilika. Alisema mradi huo ni sehemu ya mradi wa
kulinda, kuheshimu na kuhifadhi maarifa
ya asili ambao unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani(GEF) kupitia programu
za miradi midogo inayoratibiwa na shirika la maendeleo la umoja wa mataifa
(UNDP) Tanzania na ofisi ya makamu wa Rais (Mazingira).
Alisema katika mradi
huo MAIPAC hivi karibuni itazindua kitabu cha pili cha maarifa ya asili ya
jamii za Asili za Wadzabe, Datoga na
Maasai katika uhifadhi wa Mazingira, Vyanzo vya Maji na Misitu.
Afisa Maendeleo wa
halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Fauzia Omar alipongeza shirika la MAIPAC na
SYWSO kwa kutoa misaada mbalimbali kwa wilaya hiyo na kutaka waendelee kusaidia
jamii.
Aliomba mashirika
hayo kufika vijiji vyote 62 katika wilaya hiyo, kushirikiana na serikali
kusaidia miradi ya jamii lakini pia kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya
wanawake na watoto.
0 Maoni