WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa jana Juni 21, 2025 alimuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
tamasha la Grand Bunge Bonanza lililofanyika katika viwanja vya shule ya
Sekondari ya John Merlin jijini Dodoma.
Akizungumza katika
bonanza hilo, Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anatambua na
kuthamini mchango wa Bunge la Tanzania katika kuimarisha umoja, Afya na
mshikamano kupitia michezo mbalimbali.
Mheshimiwa Majaliwa
amesema kuwa tamasha hilo ni sehemu ya makakati wa bunge wa kuunga mkono
jitihada za Rais Dkt. Samia za kuhamasisha watanzania kushiriki mazoezi ya
viungo na lina mchango mkubwa katika kuhamasisha uwepo wa utamaduni wa kufanya
mazoezi ya mwili.
“Mazoezi haya
mliyoyafanya kupitia Grand Bunge Bonanza yana umuhimu mkubwa si tu kwa afya,
bali pia yanajenga urafiki na uhusiano mwema miongoni mwetu lakini pia
yanaimarisha afya ya akili na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji wa
majukumu yetu ya kila siku kwenye maeneo yetu.”
Kwa upande wake,
Naibu Spika Mussa Azzan Zungu amempongeza Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson kwa
kuasisi bonanza la bunge ambalo kwa kiasi kikubwa limekuwa likiwaleta pamoja
wabunge kushiriki michezo mbalimbali.
Naye, Mwenyekiti wa
Bunge Bonanza Festo Sanga amesema kuwa bonanza hilo ni matokeo ya Maamuzi ya
Spika wa Bunge Dkt. Tulia ya kuamua kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
kuhamaisha michezo ili kuwa na Taifa imara na lenye Afya. “Asante sana Serikali
kwa kuhamasisha wananchi kushiriki michezo.”
Kwa Upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema michezo ni moja
ya ajenda muhimu ya benki ya CRDB “Michezo si afya bali ni ajira na ni sehemu
ya kuibua vipaji mbalimbali kwenye jamii, bonanza hili ni maalum,
muhimu na lakipekee.”
0 Maoni