Sekta ya utalii
nchini Tanzania imeendelea kushuhudia mafanikio makubwa, kufuatia mikakati ya
Serikali katika kuimarisha na kutangaza vivutio vya utalii kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyowasilishwa bungeni leo Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba,
imesema idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kutoka 1,183,416 mwaka 2020
hadi 5,360,247 mwaka 2024.
Dkt. Nchemba, amesema
mapato yatokanayo na sekta hiyo pia yamepanda kutoka dola za Marekani milioni
715 mwaka 2020 hadi dola bilioni 3.9 mwaka huu, hali iliyoifanya Tanzania
kutambulika kuwa miongoni mwa nchi tatu bora barani Afrika kwa ongezeko la
mapato ya utalii.
Mafanikio hayo
yanatajwa kuwa matokeo ya juhudi mahususi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya
Sita, ikiwemo kutengeneza filamu za kimataifa kama Tanzania – The Royal Tour na
Amazing Tanzania, ambazo zimetumika kuitangaza nchi na vivutio vyake duniani
kote.
Tanzania pia imetajwa
kuwa kinara wa nchi zinazovutia watalii Afrika kwa mwaka 2024 (Africa’s Leading
Destination), huku Hifadhi ya Taifa Serengeti ikishinda tena tuzo ya hifadhi
bora duniani kwa mwaka wa tano mfululizo.
Waziri wa Fedha Dkt.
Nchemba, ameongea hayo leo Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti
Kuu ya Serikali, ambapo ameliomba Bunge ridhaa ya kukusanya na kutumia jumla ya
shilingi trilioni 56.49 kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.
Bajeti hiyo, ambayo
ni kubwa zaidi kuwahi kuwasilishwa katika historia ya nchi, inalenga kuendeleza
mageuzi ya kiuchumi, kuboresha huduma za kijamii, na kuimarisha sekta
zinazochochea maendeleo kama kilimo, viwanda, na utalii.
Kwa mujibu wa Dkt. Nchemba,
mafanikio ya utalii si tu yameongeza mapato ya Serikali bali pia yamefungua
fursa mpya za ajira kwa vijana na kuinua kipato cha wananchi katika maeneo
yanayozunguka vivutio vya utalii.
“Tumejipanga
kuendeleza mafanikio haya kwa kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ya utalii,
masoko ya kimataifa, na mafunzo kwa wadau wa sekta hii muhimu,” alisema Waziri wa
Fedha Dkt. Nchemba.
Bunge linatarajiwa kujadili bajeti hiyo katika siku zijazo, huku Watanzania wengi wakiwa na matumaini ya kuona utekelezaji wake ukiakisi ahadi ya Serikali ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wote.
0 Maoni