Serikali imesema kuwa hadi kufikia Aprili 2025, deni la taifa
limefikia shilingi trilioni 107.70, likiwa bado ndani ya viwango vya uhimilivu,
huku ikiahidi kuendelea na mikakati ya kuhakikisha haligeuki mzigo kwa uchumi
wa nchi.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/25 bungeni
leo, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kati ya kiasi hicho, deni
la nje ni shilingi trilioni 72.94 huku deni la ndani likiwa shilingi trilioni
34.76.
“Mheshimiwa Spika, tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika
Oktoba 2024 inaonesha kuwa deni la Serikali ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati
na mrefu,” alisema Dkt. Mwigulu na kuongeza: “Thamani ya sasa ya deni la
Serikali kwa Pato la Taifa ni asilimia 40.3, chini ya ukomo wa asilimia 55.
Aidha, thamani ya sasa ya deni la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 23.6 dhidi
ya ukomo wa asilimia 40, na kwa mauzo ya nje ni asilimia 123.8 huku ukomo ukiwa
asilimia 180.”
Katika kuimarisha uaminifu wa Tanzania katika masoko ya fedha ya
kimataifa, Dkt. Mwigulu alisema kampuni ya kimataifa ya Moody’s Investors
Service ilifanya tathmini Machi 2025 na kuiweka Tanzania katika daraja la B1,
sawa na ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka 2024.
“Pia, kampuni ya Fitch Ratings inaendelea na mapitio yake ya mwaka
2025 na matokeo yanatarajiwa kutangazwa hivi karibuni. Katika tathmini yake ya
mwisho Desemba 2024, Tanzania iliwekwa katika daraja la B+,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, nafasi hiyo ya nchi katika madaraja ya
kimataifa inaendelea kutoa taswira chanya ya Tanzania kimataifa, ikiwa ni bora
kuliko baadhi ya nchi nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Dkt. Mwigulu alieleza kuwa matokeo hayo yamechangiwa na juhudi za
Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan, kupitia usimamizi madhubuti wa uchumi, uimarishaji wa mazingira
ya uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa.
Katika kuhakikisha deni linaendelea kuwa himilivu, Serikali
imesema itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza
utegemezi wa mikopo, kuelekeza fedha za mikopo katika miradi ya kimkakati
inayoongeza mapato na mauzo nje ya nchi, na kuhakikisha miradi ya maendeleo
inatayarishwa ipasavyo kabla ya kuingia mikataba.
“Maafisa Masuuli wote wanaelekezwa kuzingatia maandalizi ya miradi
kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili kuepusha ongezeko la
gharama zisizo za lazima,” alisisitiza Waziri huyo.
Waziri wa Fedha,
anamewasilisha Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali, ambapo ameliomba Bunge ridhaa
ya kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 56.49 kwa Mwaka wa Fedha
2025/26.
0 Maoni