Rais wa AfDB awasili nchini kwa ziara ya siku nne

 

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayemaliza muda wake, Dkt. Akinwumi Adesina, amewasili jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Juni 12, 2025 kwa ziara ya kikazi ya siku nne ambayo itamfikisha katika mikoa mbalimbali nchini.

Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dkt. Adesina alipokelewa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo.

Katika ratiba ya ziara yake, Dkt. Adesina anatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mazungumzo hayo yanatarajiwa kugusia maeneo ya ushirikiano baina ya Tanzania na Benki hiyo, hususan katika sekta ya miundombinu, kilimo na uwezeshaji wa vijana.

Mnamo Juni 14, 2025, Dkt. Adesina na Rais Samia watashiriki hafla ya uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato pamoja na barabara ya mzunguko ya jiji la Dodoma, miradi ambayo inatekelezwa kwa msaada wa kifedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Katika hatua nyingine ya heshima, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimetangaza kumtunuku Dkt. Adesina Shahada ya Heshima ya Uzamivu (Falsafa) kwa kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya bara la Afrika, hasa kupitia mageuzi ya kilimo na uwekezaji katika miradi ya kimkakati. Hafla ya kutunuku shahada hiyo itafanyika Juni 13, 2025 jijini Dar es Salaam.

Ziara ya Dkt. Adesina inatazamwa kama fursa ya kuimarisha uhusiano wa Tanzania na taasisi hiyo kubwa ya kifedha barani Afrika, huku nchi ikiendelea kusaka fursa zaidi za uwekezaji na ushirikiano wa maendeleo.



Chapisha Maoni

0 Maoni