WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mkazo katika kulinda na
kudumisha amani nchini ili kuhamasisha maendeleo na kuziba mianya ya kuibuka
kwa migogoro miongoni mwa wanajamii.
Ametoa kauli hiyo leo
(Jumapili Juni 29, 2025) wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kufunga kongamano la Afrika Mashariki la Amani lililoandaliwa na The Islamic
Foundation, katika viwanja vya shule ya msingi Mirongo jijini Mwanza.
“Nataka niwaambie
bila amani hatuwezi kupata mafanikio yoyote, kupitia kongamano hili mmepata
nafasi ya kujadili kuhusu tunu hii ya amani, ambayo wakati wote tumeshuhudia
viongozi wa dini mkiwa kwenye majukwaa yenu mkihimiza amani miongoni mwa
wanajamii, tuishike tunu hii”.
Kadhalika, amewataka
Watanzania kuangalia kwa upana wake suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii
hasa kwa vijana. “Ni muhimu sana suala hili mkaliweka kama agenda katika
mikutano na vikao vyenu, kila kiongozi wa dini anapozungumza, suala la maadili
na mmomonyoko wa liwe ni ajenga ya kudumu.”
Amesema kuwa
mabadiliko ya teknolojia na kuiga tamaduni za mataifa ya nje imekuwa miongoni
mwa chanzo kikubwa cha mmomonyoko wa maadili. “Siku hizi vijana kuwaita wazee
kwa majina yasiyo na heshima ni kitu cha kawaida, viongozi ndio wenye jukumu la
kusimamia eneo la maadili, mkifanya hivyo tupata vijana wenye maadili mema.”
Pia Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa falsafa ya 4R ya Resilience (Ustahimilivu),
Reconciliation (Maridhiano) and Reforms (Mageuzi), Rebulding (Kujenga upya)
iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika misingi imara ya
kulinda amani. “Falsafa hii imeifanya Tanzania kuwa tulivu na salama.”
Wakati huo huo
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa jamii inapaswa kuona umuhimu wa kukuza
utamaduni wa majadiliano na maridhiano katika kushughulikia tofauti zilizopo
mingoni mwa jamii.
“Tunapaswa kujenga
jamii inayoheshimu maoni tofauti, na kuhimiza mijadala kwenye majukwaa na kwa
nafasi hii viongozi, taasisi na wanajamii mnapaswa kuwa daraja la maridhiano
badala ya kuwa vyanzo vya migawanyiko.”
Naye Mwenyekiti wa
Islamic Foundation Aref Nahdi amesema kuwa taasisi zao zitaendelea kushirikiana
na Serikali katika kuijenga Tanzania yenye haki, Amani, usawa, maendeleo na
heshima kwa wote.
Aidha, amesema kuwa
taasisi hizo zitaendelea kukemea vikali kauli zenye viashiria vya uvunjifu wa
amani, upendo na kuvunja heshima za viongozi wa kitaifa. “Kwa kufanya hivyo
inakuwa ni sehemu ya mafundisho ya dini.”
0 Maoni