Serikali imesema
kuwa inatambua kufikia usalama wa
chakula na lishe si tu kuhusu kuongezeka kwa mavuno bali ni kuhakikisha kwamba kile kinacholiwa
kinawaimarisha wananchi na kusaidia afya zao kwa kipindi kirefu.
Hiyo inatajwa kuwa
njia jumuishi iliyopo katika sera za nchi na uwekezaji unaoenda sambamba na
vipaumbele vya maendeleo ya Taifa na maono ya kufikia mifumo ya chakula
endelevu inayosaidia ustawi na mafanikio ya watu kama lilivyo lengo la
Kongamano la Kumi la Utafiti wa Kilimo, Lishe na Afya (ANH 2025).
Akifungua rasmi
Kongamano hilo Juni 23, 2025 jijini Dar es salaam kwa niaba ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
amesema kuwa nchini Tanzania kilimo kinabaki kuwa nguzo ya uchumi inayochangia
takriban asilimia 29 ya Pato la Taifa, kikiajiri zaidi ya asilimia 65 ya watu
na kuhakikisha usalama wa chakula kwa mamilioni.
“Tumeendelea kuwekeza
kimkakati katika sekta hii. Kwa mwaka huu, bajeti yetu ya Wizara ya Kilimo
imeongezeka kwa takriban asilimia 29. Kupitia programu za ruzuku za serikali na
mipango mingine ya msaada wa pembejeo, tumefikia mamilioni ya wakulima wadogo
nchini kwa mbegu bora na upatikanaji wa mbolea,” amesema Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa kupitia
Mradi wa Kujenga Kesho Bora
(BBT), umewawezesha vijana kushiriki katika kilimo cha kisasa, kuboresha huduma za ugani, na kuwekeza katika
miundombinu ya umwagiliaji ili kufanya kilimo kuwa na ufanisi zaidi, kiuchumi
na lishe ili kuwa na maendeleo bora na afya.
Kuhusu lishe
amesema ni msingi muhimu wa ajenda ya maendeleo ya kiuchumi na ya binadamu,
licha ya mafanikio yaliyopatikana amesema bado zipo changamoto kadhaa akitolea mfano Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO)
ikionesha kwamba takriban asilimia 30 ya watoto barani Afrika wenye umri wa
chini ya miaka mitano bado wanakabiliwa na ukosefu wa ukuaji, wakati kiwango
cha kuwa na uzito kupita kiasi kinakua. Aidha, watoto wengi na wanawake wenye
umri wa kuzaa wanaendelea kukumbwa na ukosefu wa virutubisho.
Amesema katika
kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imepunguza uratibu wa sekta nyingi
kupitia Mpango wa Kitaifa wa Hatua za Lishe (NMNAP), ambao sasa upo katika
awamu yake ya pili ili kushughulikia aina zote za utapiamlo katika makundi yote
ya watu. Vilevile, Tanzania inakuza uzalishaji na matumizi ya mazao yenye
virutubisho hasa katika maeneo ya vijijini na yasiyo na mvua kulingana na hali
za kilimo kama sehemu ya mabadiliko ya mifumo ya chakula ya ndani na kuimarisha
ajenda ya nchi.
Kwa upande wa afya,
Dkt. Biteko amesema Serikali inaendelea na dhamira yake ya ushirikiano katika
masuala ya afya ulimwenguni, huku ikifanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu,
utoaji wa huduma, na mageuzi ya mifumo ya afya pamoja na kuongeza idadi ya
vituo vya afya kwa takriban asilimia 7 tangu mwaka 2021.
“Serikali imeongeza
idadi ya wafanyakazi wa afya kwa kuajiri takriban wafanyakazi wa afya wa jamii
137,000 katika ngazi za msingi na kuongeza mikakati ya afya ya kidijitali.
Tunashughulikia changamoto zinazohusiana na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na
magonjwa ya kuambukiza na afya ya mama na mtoto kupitia mikakati mbalimbali
ikiwemo kutumia wafanyakazi wa afya wa jamii, wadau wengine na kampeni za
kitaifa ili kuongeza uelewa na kuongeza uwezo wa kugundua mapema na kuzuia
katika ngazi zote, ” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, amesema
Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wengine katika sekta ya afya, lishe
na kilimo sambamba na kufaidika na
ushirikiano imara na wa kimkakati na washirika wa kimataifa na taasisi nyingine
za kikanda na za kimataifa. Pia, Tanzania ipo tayari kujifunza na kuongoza pale
inapowezekana huku akiwaasa washiriki wa Kongamano hilo kushiriki ipasavyo ili
kuwa na hoja na sera ambazo zitabadilisha mifumo ya chakula kwa afya bora na
ustawi.
Amesisitiza “Tanzania
pia inaendelea kushiriki katika majadiliano ya mifumo ya chakula ya bara na
kimataifa, ikichangia katika Ajenda ya 63 ya Umoja wa Afrika, Mfumo wa CAADP na
UN.”
Balozi wa Uingereza
nchini Tanzania, Mhe. Marianne Young amesema kuwa nchi yake itaendelea kuwa
mshirika muhimu kwa Tanzania na kuwa na mafanikio ya muda mrefu katika sekta
za lishe, afya na kilimo.
“ Tumesaidia wanawake wajawazito milioni 6.7
kwa kuwapatia virutubisho lishe, kubadili na
mitazamo ya jamii kuhusu usafi na
kusadia ukarabati wa miundombinu ya upatikanaji wa maji safi vijijini kwa watu milioni 5.5, ” amesema
Balozi Young.
Naye, Mkurugenzi wa
Taasisi ya Kisayansi ya ANH (Agriculture, Nutrition and Health Academy) Bw. Joe
Yates amesema kuwa kila mwaka Kongamano la ANH hufanyika katika nchi za Afrika
na Asia ambalo huwaleta pamoja watafiti, wanasayansi, watunga sera na wadau
mbalimbali wa masuala ya kilimo, lishe na afya.
Lengo likiwa ni
kujadili kwa pamoja, kubadilishana fikra na uzoefu na kubaini masuala mbalimbali
ya kisayansi kwa ajili ya kuchagiza katika kuunda sera za maendeleo ya kilimo,
lishe na afya na kwa mwaka 2025 limefanyika nchini kwa kushirikiana na Chuo
Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).
0 Maoni