WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa ameziagiza taasisi za Serikali ambazo hazijajiunga na mfumo wa
kielektroni utakaowezesha mifumo ya Serikali kuwasiliana (GovESB) kujiunga na
mfumo huo ifikapo Julai 30 mwaka huu ili kuendana na mabadiliko ya
teknolojia katika kurahisisha
upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Ametoa maagizo hayo
leo Jumatatu (Juni 23, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika
viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma.
“Taasisi zote za umma
ambazo hazijajiunga na mfumo huu mwisho ni Julai 30 mwaka huu, wote muwe
mmeshaingia pale GovESB, huu ni msisitizo ambao ulitolewa na Mheshimiwa Rais
Dkt. Samia pindi eGA watakapokamilisha kila taasisi ipeleke mfumo wake, idadi
ya taasisi zilizounganishwa ni chache, hakuna gharama na hutakiwi kupanga
bajeti.”
Ameongeza kuwa mfumo
huo unafaida kubwa katika utumishi wa umma kwani utasaidia kurahisisha
utendaji, kutoa taarifa kwa wakati, kuondoa makosa ya kibinadamu katika
kuwahudumia wananchi pamoja na kuwabana wala rushwa. “Nimefurahi kujulishwa
kwamba jumla ya mifumo 223 kutoka kwenye taasisi 185 imeunganishwa na
kusomana”.
Aidha, Mheshimiwa
Majaliwa ametoa wito kwa taasisi zote za umma zenye mifumo na zinazoendelea
kubuni mifumo zihakikishe mifumo hiyo inasomana na inaweza kubadilishana
taarifa kupitia mfumo huo wa GovESB ikiwa ni njia mojawapo ya kuendelea
kuboresha huduma za Serikali.
Kadhalika Mheshimiwa
Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kuhakikisha mifumo
iliyounganishwa inaendelea kubadilishana taarifa. “Lakini pia kila anayeingia
jiridhishe kuwa anaweza kuwasiliana na wengine wote waliomo ndani, mmenieleza
na mmesema kwamba ndivyo ilivyo, nasisitiza kwamba hakikisheni hiyo mifumo
inasomana na inabadilishana taarifa.”
Katika hatua
nyingine, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa wito kwa watumishi wa umma kuzingatia
miiko na maadili ya utumishi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingitia
Sera na Sheria kwa manufaa na maendeleo ya Taifa letu. “Nitumie nafasi hii
kuwapongeza sana watumishi wote wa umma nchini, niwahikishie kuwa serikali ya
awamu ya sita iko pamoja nanyi. “Fanyeni hivyo kwa ajili ya manufaa na
maendeleo ya Taifa letu”.
Kwa upande wake,
Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
George Simbachawene amesema Tanzania imetambulika kimataifa ambapo mwaka 2022
Benki ya Dunia ilifanya utafiti kuhusu ukomavu wa matumizi ya teknolojia
duniani katika utoaji wa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi.
Amefafanua kuwa
ripoti ya utafiti huo iliyotolewa Machi, 2023 ilibanisha kuwa Tanzania
imefanikiwa kupanda daraja kutoka kundi B hadi kundi A na kushika nafasi ya 26
duniani, nafasi ya 2 Afrika na nafasi ya kwanza katika nchi za Afrika
Mashariki.
Katika tukio hilo,
Mheshimiwa Majaliwa alizindua mifumo miwili ambayo ni Mfumo wa kielektroni
unaowezesha mifumo ya Serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa ujulikanao
kama Government Enterprises Service Bus (GovESB) Pamoja na Mfumo wa e-Wekeza
unaomuwezesha Mtumishi wa Umma kuwekeza katika Mfuko wa Faida (Faida Fund).
Siku ya Utumishi wa
Umma husherehekewa Juni 23 kila mwaka na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kwa
lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya nchi zao na
Bara la Afrika kwa ujumla.
0 Maoni