Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametangaza kuwa
atalivunja rasmi Baraza la Kumi la Wawakilishi ifikapo tarehe 13 Agosti 2025.
Akizungumza katika
kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichofanyika leo, tarehe 23 Juni 2025,
Chukwani, Mkoa wa Mjini Magharibi, Dkt. Mwinyi amesema kuwa hatua hiyo ni kwa
mujibu wa Kifungu cha 92 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Katika hotuba yake,
Rais Dkt. Mwinyi ameelezea kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika kipindi
cha miaka mitano ya uongozi wake ni pamoja na kuimarika kwa uchumi, kuendelezwa
kwa amani, na mafanikio ya kuwaleta wananchi pamoja bila kujali rangi, asili,
jinsia, dini au itikadi za kisiasa. Pia amesisitiza kuendelea kuwepo kwa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kuhusiana na
Muungano, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa mafanikio yamepatikana katika
kuimarisha Muungano wa Tanzania kisiasa, kiuchumi na kijamii, tangu kuanzishwa
kwa utaratibu wa kushughulikia hoja za Muungano mwaka 2006, ambapo hoja 26
zimejadiliwa na 22 kupatiwa ufumbuzi.
Akihitimisha hotuba
yake, Rais Dkt. Mwinyi amewasisitiza wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya
kupiga kura na kushiriki uchaguzi kwa kudumisha amani kabla, wakati, na baada
ya uchaguzi. Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia na
viongozi wa dini kutekeleza wajibu wao wa kikatiba katika kipindi hiki muhimu.
Amesema kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania (SMT) kupitia Tume za Uchaguzi za ZEC na NEC, inaendelea
na maandalizi ya uchaguzi kwa misingi ya haki na sheria.
Mapema, Spika wa
Baraza la Wawakilishi, Mhe. Zubeir Ali Maulid, alitangaza rasmi kumalizika kwa
maisha ya Baraza la Kumi la Wawakilishi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, na
kumshukuru Rais wa Zanzibar kwa ushirikiano wake pamoja na kuwashukuru wajumbe
wa Baraza kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.





0 Maoni