Serikali imefanikiwa
kuajiri jumla ya Wataalam wa kada ya Ustawi wa Jamii 1,546, ambao kwa sasa
wamepangiwa kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya kusaidia
kukabiliana na tatizo la Afya ya Akili na Ustawi wa Jamii.
Hayo yamesema leo
Juni 24 bungeni Jijini Dodoma katika
kipindi cha maswali na majibu na Mhe. Dkt. Festo Dugange, Naibu Waziri Ofisi ya
Rais – TAMISEMI kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ofisi ya Rais –
TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akijibu swali la Mhe. Hawa Mwaifunga,
Mbunge wa Viti Maalum.
Mhe. Mwaifunga
alitaka kujua mpango wa Serikali kuajiri Wanasaikolojia ngazi ya Kata ili
kusaidia kukabiliana na tatizo la Afya ya Akili.
Mhe. Dkt. Dugange
ameongeza kuwa, hatua hiyo ya kuajiri wataalamu hao ni sehemu ya juhudi za
kuboresha huduma za kisaikolojia kwa wananchi wenye uhitaji ambayo ni muhimu
katika kuhakikisha kuwa huduma za afya ya kiakili zinapatikana kwa urahisi na
kwa ufanisi kwa jamii nzima.
“Kwa mujibu wa Muundo
wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2022, huduma hizo hutoa msaada kwa
watu wanaohitaji, zimepangwa kutolewa na Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na
Lishe. Wataalam hawa wataanza kuelekeza huduma zao kupitia Makao Makuu ya
Halmashauri na ngazi mbalimbali katika mamlaka husika,” alisema.
Aidha, Serikali
imesema itaendelea kuajiri wataalam wa kada ya Ustawi wa Jamii, kwa malengo ya
kuhakikisha Halmashauri zilizokabiliwa na upungufu wa wataalam zinaweza kupata
msaada wa kutosha katika kutoa huduma hizi muhimu kote nchini.
Na. OR - TAMISEMI
0 Maoni