Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, ameongoza kikao cha Baraza la Uongozi la Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Barani Afrika (African Forestry and Wildlife Commission - AFWC) kinachofanyika kwa siku tatu jijini Accra, Ghana.
Kikao hicho
kimewakutanisha viongozi waandamizi kutoka nchi wanachama wa Shirika la Chakula
na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa lengo la kujadili maendeleo, changamoto
na mikakati ya pamoja ya kuimarisha usimamizi endelevu wa misitu na wanyamapori
barani Afrika.
Pia kinatumika
kuandaa mkutano wa 25 wa Kamisheni hiyo, unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka
huu sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Misitu na Wanyamapori Afrika.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi, Profesa Silayo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo na Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Misitu (Committee on Forestry – COFO)
alisema Kamisheni hiyo ni jukwaa muhimu kwa nchi za Afrika kujadili sera,
mafanikio na changamoto zinazokabili sekta ya misitu na wanyamapori.
Alisisitiza kuwa AFWC
pia ina jukumu la kushauri FAO na nchi wanachama kuhusu sera, mipango na mbinu
bora za usimamizi wa rasilimali hizo kwa kuzingatia mahitaji ya kikanda.
Aliongeza kuwa
Kamisheni hiyo huchochea ushirikiano wa kikanda baina ya nchi za Afrika katika
nyanja za uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu na wanyamapori, na hufuatilia
utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kama vile Mkataba wa Umoja wa Mataifa
kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), Mkataba wa Bioanuwai (CBD), na Mpango
wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa (REDD+).
Aidha, Kamisheni
huwasilisha msimamo wa pamoja wa Afrika katika maamuzi ya Kamati ya Kimataifa
ya Misitu (COFO).
Profesa Silayo
alibainisha kuwa kikao hicho ni fursa adhimu kwa bara la Afrika kufanya
tathmini ya utekelezaji wa sera mbalimbali na kuweka mikakati ya kuimarisha
ushirikiano wa kikanda kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo.
Alisisitiza kuwa
katika kipindi hiki cha changamoto za kimazingira, ongezeko la watu na
shinikizo kwa rasilimali asilia, bara la Afrika linahitaji kuwa na msimamo
mmoja na hatua madhubuti za pamoja.
Miongoni mwa viongozi
walioungana na Profesa Silayo katika kikao hicho ni Abbey Haile Gabriel,
Mkurugenzi Msaidizi wa FAO Kanda ya Afrika; Pierre Taty, Mwenyekiti wa Kamati
ya Kimataifa ya Misitu (COFO); Profesa Labode Popoola, Katibu Mtendaji wa
Jukwaa la Misitu Afrika (AFF); na Edward Kilawe, Katibu wa Kamisheni ya Misitu
na Wanyamapori Afrika.
Kamisheni ya Misitu
na Wanyamapori Afrika (AFWC) ni chombo cha kikanda kilichoanzishwa chini ya FAO
kwa madhumuni ya kuratibu, kushauri na kuendeleza usimamizi endelevu wa misitu
na wanyamapori katika bara la Afrika. Makao yake makuu yapo katika Ofisi za FAO
Kanda ya Afrika jijini Accra, Ghana. Kwa sasa, Kamisheni hiyo inaongozwa na
Tanzania kupitia Profesa Silayo, hatua inayoakisi mchango mkubwa wa nchi katika
majukwaa ya kimataifa ya uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya
rasilimali za misitu.
Na. Mwandishi Wetu -
Accra Ghana
0 Maoni