WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inawaamini na inathamini
mchango wa viongozi wa dini wa madhehebu yote.
Amesema
serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano kati yake na viongozi hao ili
kujenga amani, mshikamano na ustawi wa jamii ya watanzania.
"Tunaamini
mtaendeleza jukumu la kuwasihi watanzania waone umuhimu wa kila mmoja kuwa
sehemu ya mchango wa kulifanya taifa hili kuwa tulivu na kuimarisha mshikamano
miongoni mwetu."
Ameyasema hayo leo
(Jumamosi Juni 7, 2025) alipokuwa mgeni rasmi katika Sala na Baraza la
Eid Al Adha iliyofanyika katika Msikiti wa Mohamed VI Kinondoni, Dar es Salaam.
Amesema viongozi wa
dini wanayo nafasi kubwa ya kuwajenga waumini wao kuwa na staha, ustaarabu,
uvumilivu na kutambua kuwa wao ni miongoni mwa wanajamii na kushiriki katika
shughuli za kimaendeleo.
"Kwa upande wa
serikali tunaendelea kujenga misingi ya mshikamano kati ya waumini wa dhehebu
moja na dhehebu jingine, tukiwa tunaamini kuwa dini zimeendelea kuifanya nchi
hii kuwa nchi ya amani wakati wote."
Kadhalika ametoa wito
kwa watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo nchini ili nchi
iendelee kupata ustawi.
Amesema ni vyema kuwa
na uwezo wa kukemea vitendo vyovyote ambavyo vinaashiria kutishia amani
nchini.
Aidha, amewasihi
watanzania kuendelea kuwaombea viongozi wa kitaifa hususan Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ili Mungu ampe nguvu
na afya ya kuendelea kuliongoza taifa hili.
Kadhalika,
amewapongeza waislamu waliofanikiwa kutimiza ibada ya Hijja huku akitoa wito
kwa waislamu waliopo nchini kuendelea kuwaombea warudi salama.
"Tuendelee
kuwaombea wenzetu wakamirishe ibada hiyo, kwetu sisi ni baraka kwa sababu hata
sisi wanatuombea."
Pia amewapongeza
viongozi wa dini kuendelea kutoa mafunzo kwa vijana wadogo ili wakue kwa
kuzingatia misingi imara ya kuendeleza dini na maadili yake.
"Dini zina
ujenzi mkubwa kwa muumini kiimani na tunapowajenga waumini wetu kiimani
tuwaingizie imani yenye manufaa kwa taifa".
Naye, Kaimu Mufti wa
Tanzania Sheikh Ali Khamis Ngeruko, ametoa wito kwa watanzania kuwa makini
wakati wa uchaguzi ili wachague viongozi wenye weledi kwa kumpima namna anavyo
wasilisha sera zake.
"Dunia imekuwa
na changamoto kubwa ya watu wenye afya ya akili hivyo tunapo wachagua viongozi
tuwachague watu ambao afya zao za akili ziko kwenye kiwango cha juu na
kinachoridhisha."
Kwa upande wake,
Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Alhaj Nuru Mruma, amesema
Baraza hilo linawahimiza watanzania kuendelea kuilinda amani iliyopo nchini ili
kutoa nafasi kwa shughuli za kimaendeleo kufanyika.
"Baraza linatoa
wito kwa kila Mtanzania kwa nafasi yake kulinda na kudumisha amani, kwani bila
amani hakutakuwa na maendeleo yoyote katika jamii".
0 Maoni