RC Mtambi Azindua Shule Mpya ya Sekondari Muhoji

 

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Kanali Mstaafu Evans Mtambi, leo amezindua rasmi shule mpya ya sekondari ya Muhoji iliyopo katika Kijiji cha Muhoji, Kata ya Bugwema, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.

Uzinduzi huo umefanyika mbele ya mamia ya wananchi wa Kata ya Bugwema inayojumuisha vijiji vinne vya Bugwema, Kinyang’erere, Masinono na Muhoji, ambapo shule hiyo mpya inakuwa sekondari ya pili katika kata hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mtambi amesema ujenzi wa shule hiyo ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu nchini.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu kwa Watanzania wote. Hii ni sehemu ya juhudi za Serikali kupeleka maendeleo hadi ngazi ya kijiji,” alisema RC Mtambi.

Wananchi wa Kata ya Bugwema pamoja na viongozi wao walitumia jukwaa hilo kueleza kwa sauti moja kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ndiye chaguo lao pekee kuendelea kuiongoza nchi kutokana na kazi kubwa anayofanya hususan kwenye sekta ya elimu.

Ujenzi wa shule hiyo ulianza mwezi Desemba 2022 kupitia michango mbalimbali iliyokusanywa kwenye harambee iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo ujenzi, shule hiyo umegharimu jumla ya Shilingi 175,346,955 hadi hatua iliyofikiwa, huku Serikali Kuu ikitoa Tsh 75 milioni na Mfuko wa Jimbo Tsh 24.4 milioni.



Chapisha Maoni

0 Maoni