Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kushirikiana kwa dhati katika kuchukua hatua za pamoja ili kuendeleza uchumi wa bahari, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kulinda bioanuwai ya baharini.
Dkt. Mpango ametoa
wito huo leo wakati akihutubia Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu
Bahari (UNOC3), unaoendelea katika Jiji la Nice, nchini Ufaransa, ambapo
alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan.
Katika hotuba yake,
Makamu wa Rais amesema kuwa ni muhimu kwa mataifa yote kushikamana kimataifa na
kuwekeza kwa namna endelevu ili kuimarisha ulinzi wa bahari na kuhakikisha kuwa
rasilimali zake zinatumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Tunapaswa kuchukua
hatua madhubuti, sio tu kwa ajili ya mazingira bali pia kwa ajili ya ustawi wa
kiuchumi wa mataifa yetu. Bahari ni chanzo muhimu cha maisha, ajira na chakula
kwa mamilioni ya watu duniani,” alisema Dkt. Mpango.
Akieleza juhudi za
Tanzania katika kulinda mazingira ya baharini, Dkt. Mpango alibainisha kuwa
nchi hiyo imeongeza maeneo ya hifadhi ya bahari kwa lengo la kufikia asilimia
20 ya eneo la maji ifikapo mwaka 2030.
Aidha, alieleza kuwa
Tanzania inaendelea na utekelezaji wa mikakati ya uhifadhi na usimamizi
shirikishi unaoongozwa na jamii, kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo
wananchi wa maeneo ya pwani. “Ushirikiano huu umeongeza hamasa ya jamii
kuilinda na kuithamini bahari, kwa kuwa wanajiona kuwa ni sehemu ya suluhisho,”
aliongeza.
Mkutano huo wa UNOC3
unalenga kuunganisha juhudi za kimataifa katika kukabiliana na changamoto
zinazoikabili bahari ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na
uvuvi haramu.
Tanzania ni miongoni
mwa mataifa yanayopakana na Bahari ya Hindi, ikiwa na fursa na changamoto
nyingi zinazohusiana na matumizi ya rasilimali za baharini, hivyo kushiriki
kwake katika mikutano ya namna hii kunalenga kuimarisha ushiriki na ushawishi
wa nchi katika ajenda za kimataifa kuhusu bahari.
0 Maoni