Mvutano mkali kati ya
familia ya aliyekuwa rais wa Zambia, serikali na chama chake cha kisiasa cha
Patriotic Front (PF) umeacha waombolezaji katika hali ya sintofahamu kuhusu
namna ya kumuenzi Rais wa zamani Edgar Lungu.
Serikali imetangaza
kuwa kutakuwa na mazishi ya kitaifa na kusema kuwa eneo rasmi la maombolezo
litakuwa katika jengo linalomilikiwa na serikali mjini Lusaka. Hata hivyo,
chama cha PF kimekataa mpango huo na kuwaelekeza waombolezaji kufika makao
makuu ya chama hicho badala yake.
Kwa upande wake,
familia ya Lungu imesema haina pingamizi kuhusu kuwepo kwa mazishi ya kitaifa,
lakini imesisitiza kuwa ni wao watakaochagua nani ataongoza shughuli hiyo, kwa
mujibu wa wakili wa familia, Makebi Zulu, alivyoiambia BBC.
Edgar Lungu, ambaye
aliongoza Zambia kuanzia mwaka 2015 hadi 2021, alifariki dunia Alhamisi
iliyopita. Kifo chake akiwa na umri wa miaka 68 kimewaacha Wazambia wengi
wakiwa na mshangao na huzuni.
0 Maoni