Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemhakikishia Jaji Mkuu mpya wa
Mahakama ya Tanzania, George Masaju, kuwa hatabaki peke yake katika kutekeleza
majukumu ya mhimili huo muhimu wa dola, akiahidi kushirikiana naye kwa karibu
katika nyakati zote – hasa anapohitaji msaada.
Rais Samia alitoa
kauli hiyo leo Jumapili, Juni 15, 2025, wakati wa hafla ya kumuapisha Jaji Mkuu
Masaju iliyofanyika Ikulu, jijini Dodoma.
“Kwa Jaji Mkuu mpya,
kwanza nikupongeze na pia nikupe pole, maana mzigo huu si mdogo, una kazi
kubwa ya kufanya,” alisema Rais Samia kwa sauti ya matumaini na mshikamano.
Katika kumtia moyo
kiongozi huyo wa Mahakama, Rais Samia alitoa mfano wa ndege iliyoko angani
inayokaribia kuishiwa mafuta, akisisitiza kuwa ni vyema kusimama kwa muda na
kujaza tena nguvu ili safari iendelee.
“Nataka nikupe mfano
mmoja tu,” alisema Rais. “Ndege ikiwa angani na mafuta yakikaribia kuisha,
haipaswi kulazimisha kutua kwa heshima, bali kutafuta kiwanja cha karibu, jaza
mafuta, uruke tena. Na unapohitaji kujaza mafuta hiyo ndege yako, niwe mimi
mtumishi wako wa kukuwekea yale mafuta, ili uweze kuruka tena na safari
iendelee.”
Kauli hiyo ya Rais
Samia imeonekana kugusa wengi waliohudhuria hafla hiyo, ikionesha dhamira yake
ya kuimarisha mahusiano kati ya mihimili ya dola, huku akionyesha wazi kuwa
yuko tayari kuwa bega kwa bega na Jaji Mkuu katika kusimamia haki na sheria
nchini.
George Masaju
aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania hivi karibuni, akichukua
nafasi hiyo muhimu katika kipindi ambacho mfumo wa utoaji haki unaendelea
kufanyiwa maboresho mbalimbali chini ya serikali ya awamu ya sita.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Mhe. Jaji George
Mcheche Masaju kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kwenye hafla iliyofanyika
Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 15 Juni, 2025.
Picha ya matukio mbalimbali
kwenye hafla ya uapisho wa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Jaji George
Mcheche Masaju, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma
tarehe 15 Juni, 2025.
0 Maoni