Serikali imeingia makubaliano na nchi mbalimbali ili kurahisisha utaratibu wa viza ambapo raia wa nchi 71 hawahitaji viza wanapoingia nchini.
Kwa sasa watalii
kutoka mataifa mengi zaidi duniani wanaruhusiwa kupata visa wanapowasili (visa
on arrival) kwenye viwanja vya ndege vya kimataifa kama Julius Nyerere (Dar es
Salaam), Kilimanjaro na Zanzibar.
Haya yamebainishwa na
Naibu Waziri wa maliasili na utalii Mhe. Dunstan Kitandula(Mb) alipokuwa
akijibu swali la Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya aliyetaka kujua ni jitihada gani
zimefanyika kurahisisha upatikanaji wa VISA kwa Watalii wenye uraia tofauti
wanaokuja nchini kwa mwitikio wa Tanzania the Royal Tour.
Aidha, Mhe. Kitandula
aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuboresha utaratibu wa utoaji wa viza nchini
ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani. Mathalan, Serikali kupitia
Idara ya Uhamiaji imeanzisha mfumo wa maombi ya viza kwa njia ya mtandao
(e-Visa) unaowawezesha watalii kuomba viza popote walipo duniani bila
kulazimika kufika ubalozini.
“Halikadhalika,
Serikali imeboresha Kanuni za Uhamiaji za mwaka 2023 (GN 428) ambapo kwa sasa
watalii wanaotumia Visitors Pass wanaruhusiwa kutembelea Nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki na kurejea Tanzania bila hitaji la kuomba upya pasi ya kuingia
nchini,” alisema Mhe. Kitandula.
Suala la visa lina
uhusiano wa moja kwa moja na sekta ya utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii
imeimarisha ushirikiano na Wizara ya Mambo ya Ndani, hususan Idara ya Uhamiaji,
katika nyanja mbalimbali ikiwemo ukusanyaji wa takwimu za watalii na kuwa na
mikakati ya pamoja ya kuvutia watalii na fursa za uwekezaji.
Aidha, siku za hivi karibuni, Wizara kupitia
Chuo cha Taifa cha Utalii imetoa mafunzo ya Huduma kwa Wateja na Ukarimu kwa
Maafisa wa Jeshi la Uhamiaji ili kuboresha huduma zinazotolewa kwa wageni
wanaoingia nchini, ikiwemo watalii.
Na. Anangisye Mwateba
- Dodoma
0 Maoni