Ofisi ya Rais –
TAMISEMI imewataka Makatibu Tawala wasaidizi sehemu za mipango, uratibu, uchumi
na uzalishaji, wakuu wa idara za mipango na uratibu na waweka hazina wa
halmashauri kubuni miradi ya maendeleo kwa kuzingatia mtaji wa rasilimali
walizonazo katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa
tarehe 6 Juni, 2025 mkoani Dodoma na
Mkurugenzi wa Idara ya Tawala za Mikoa Bi. Beatrice Kimoleta kwa niaba ya
Katibu Mkuu OR – TAMISEMI, wakati akihitimisha mafunzo ya uendeshaji na
usimamizi wa miradi ya maendeleo yaliyotolewa kwa muda wa siku nne kwa
maafisa hao yakiwa na lengo la
kuwajengea uwezo zaidi kabla ya kuanza kutekelezwa kwa bajeti ya Serikali ya
mwaka 2025/2026.
Bi. Kimoleta amesema
imani ya Serikali baada ya mafunzo hayo ni washiriki kuwa wabunifu, kila mkoa
na halmashauri hatua itakayopimwa kwa kuangalia namna maandiko ya uanzishwaji
wa miradi ya vyanzo vipya vya mapato yalivyozingatia ubunifu na mtaji wa
rasilimali walizonazo katika maeneo husika.
“Hatutegemei tena
kuona kila halmashauri inawasilisha andiko la kujenga vituo vya mabasi
(stendi) yaani halmashauri zaidi ya 80
nyote mna wazo moja, tunachokiamini kuanzia sasa ni kuona maandiko yenye mawazo
tofauti tofauti hasa yaliyozingatia kuwa eneo hili tuna rasilimali hii
tukifanya mradi fulani utakuwa na tija kwa maendeleo ya jamii yetu,”
alisema Kimoleta.



0 Maoni