NHC Kubadilisha Muonekano Kariakoo kwa Kujenga Maghorofa Mapya

 

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limepanga kubadili kabisa sura ya eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, kwa kubomoa nyumba zake zote za zamani na kujenga maghorofa ya kisasa yenye urefu wa kuanzia ghorofa 10 na kuendelea.

NHC imepanga kuotesha viota vya maghorofa Kariakoo katika kipindi cha miaka mitatu ili kuliongezea thamani eneo hilo ambalo ni kitovu cha biashara na kuongeza mapato ya shirika  kutokana na majengo ya zamani kuwaingizia mapato kidogo.

Mpango huo wa NHC wa uboreshaji mji kwa kuvunja majengo ya zamani na kujenga mapya  umetangazwa mapema wiki hii na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Bw. Hamad Abdallah Hamad, katika kikao chake na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.

“Niwapeni mfano hapa tulipo (Morocco Square) tulikuwa na majengo mawili ambayo yalikuwa yanatuingizia kiasi cha shilingi milioni mbili kwa mwezi, lakini sasa baada ya ujenzi huu tunaingiza zaidi ya shilingi milioni 600 kwa mwezi,” alisema Bw. Hamad.

Amesema kutokana na mapato wanayopata baada ya kujenga majengo mapya NHC itabomoa majengo yake yote ya zamani eneo la Kariakoo na kujenga majengo ya ghorofa 10 na kuendelea, ambapo katika miaka mitatu hakuta kuwa tena majengo ya zamani ya shirika hilo Kariakoo.

Akizungumzia ushirikishaji wa sekta binafsi, Bw. Hamad alisema kuwa kufuatia dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kufungua uchumi na kushirikisha sekta binafsi ambayo ni injini ya maendeleo, NHC ilifanya marekebisho ya Sera ya Ubia, iliyozinduliwa rasmi Novemba 16, 2022, jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa, kufuatia utekelezaji wa sera hiyo, sekta binafsi imekuwa ikishiriki kikamilifu katika miradi ya ujenzi wa majengo ya matumizi mbalimbali. Hadi sasa, miradi 21 yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 351 inaendelea kutekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam (17), Mwanza (3) na Iringa (1).

Aidha, Bw. Hamad alieleza kuwa hadi kufikia Mei 15, 2025, NHC imefanikiwa kukarabati na kuboresha nyumba 3,004 katika majengo 205, huku ukarabati wa nyumba nyingine 1,546 katika majengo 45 ukiendelea katika mikoa mbalimbali nchini.

Ameeleza kwamba ukarabati huu ni endelevu na nyumba zote za Shirika zinatarajiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa ifikapo 2026/27.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah Hamad akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam.

Chapisha Maoni

0 Maoni