WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na
Misheni Maalum ya Umoja wa Afrika ya Kutathmini Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu
utakaofanyika Oktoba, 2025 (Pre-election assessment mission - PAM), Misheni
hiyo iliongozwa na Dkt. Phumzile Mlambo-Ngcuka; Makamu wa Rais Mstaafu wa
Jamhuri ya Afrika Kusini akiambatana na Wajumbe wengine takribani 16.
Lengo la Misheni hiyo
ni kutathmini maandalizi ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na hali ya kisiasa
ilikuhakikisha misingi ya demokrasia inafuatwa kama ilivyoainishwa kwenye
Mkataba wa Afrika kuhusu Demokrasia Chaguzi na Utawala (African Charter on
Democracy, Elections and Governance.
Katika mazungumzo na
wajumbe wa Misheni hiyo, yaliyofanyika jana Juni 17, 2025 katika Ofisi ndogo ya
Waziri Mkuu, Magogoni Jijini Dar es Salaam, Dkt. Phumzile amebainisha kuwa
Misheni hiyo imeridhishwa na maandalizi
yanayoendelea kufanyika kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
“Tumefurahishwa pia kuona kuna idadi kubwa ya
wadau wa siasa nchini na kuridhishwa na mageuzi makubwa hususan ya mifumo na
Sera yaliyofanywa na Serikali katika kipindi cha hivi karibuni kuhakikisha
kiwango kikubwa cha Wananchi wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi.”
Aidha, Dkt. Phumzile amebainisha kuwa Misheni
imefurahishwa kuona kuna idadi kubwa ya ushiriki wa wanawake katika masuala ya
siasa nchini. “Hii ni ishara nzuri kuelekea kuwa na uwiano wa 50/50 katika
Uongozi na masuala ya siasa.”
Pamoja na hayo, imebainishwa kuwa kama ilivyo
kwa miaka iliyopita, wanategemea Tanzania itaendelea na utamaduni wake wa
kufanya uchaguzi kwa amani “Tumezoea Tanzania kuwa na uchaguzi wa amani hivyo
tunaamini itakuwa hivyo pia wakati huu” amesema Dkt. Phumzile.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Majaliwa ameihakikishia
Misheni hiyo kuwa Tanzania imejipanga kufanya uchaguzi huru, haki na amani kama
ilivyo miaka yote.
0 Maoni