Kufuatia maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imetumia fursa hiyo kutangaza vivutio vya utalii kwa wananchi pamoja na wadau wa utalii waliotembelea banda NCAA lililopo kwenye Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wananchi wa Mkoa wa
Dodoma na Mikoa mingine waliofika kwenye banda la NCAA wanapata elimu na ufahamu juu ya shughuli mbalimbali
zinazofanywa na NCAA kwenye Utalii, Uhifadhi na Maendeleo ya jamii huku wengi
wakionekana kuvutiwa zaidi na vivutio vya Utalii vinavyopatikana Hifadhi ya
Ngorongoro kama Bonde la kreta ya Ngorongoro, nyayo za Laitole, bonde la Olduvai George, Kreta ya Empakai, Mchanga unaohama na vivutio
vingine.
Akizungumza katika
maonesho hayo, Afisa Utalii kutoka idara ya Huduma za Utalii na Masoko, Joseph
Mzaga alieleza kuwa maadhimisho hayo ya wiki ya utumishi wa umma
yamewakutanisha na wadau mbalimbali na imekuwa fursa kwao kutangaza vivutio vya
utalii ambako wananchi wameonekana kuwa na shauku ya kutembelea hifadhini hapo.
“Tumepokea wageni
mbalimbali walioweza kufika kwenye banda letu ambao wengi wao walitamani
kufahamu zaidi kuhusiana vivutio vya utalii, namna ya kufika hifadhini,
viingilio na taarifa zingine Muhimu za kuwasaidia kwa ajili ya maandalizi ya
safari zao,” alisema Mzaga.
Kwa upande wake, Bi.
Agatha Antony ambaye ni mkazi wa Mkoa wa Dodoma aliyetembelea banda la NCAA
alieleza kuwa maonesho hayo yamekuwa msaada mkubwa kwake na wenzake wanaopanga
kutembelea Ngorongoro, kwa kuwa wamepata taarifa muhimu kuhusu gharama za
kuingia hifadhini, njia za usafiri, na mambo ya kuzingatia kabla ya safari,
jambo ambalo litawasaidia kujipanga vizuri na kuongeza hamasa kwao.
“Mimi pamoja na
wafanyakazi wenzangu kutoka taasisi ya Pharma Afrika tunajiandaa na safari ya
kutembelea hifadhi yaa Ngorongoro na leo nimefurahi zaidi kwani nimeweza kufika
hapa na nimepata taarifa ambazo zitatusaidia kwenye maandalizi yetu mfano
viingilio, usafiri na vivutio ambavyo tutaweza kuvitembelea,” alisema Agatha.
Wiki ya utumishi wa
Umma huadhimishwa kila mwaka kuanzia Juni 16 hadi 23, ikiwa ni sehemu ya
kutambua mchango wa watumishi wa Umma katika maendeleo ya Taifa ambapo kwa
mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Himiza Matumizi ya Mfumo wa Kidijitali
Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji.”
Na. Philomena Mbirika
- Dodoma
0 Maoni