Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt.Samia Suluhu
Hassan, Juni, 19 2025 alizindua daraja la “JP Magufuli” ambalo hapo awali
lilifahamika kama Kigongo- Busisi lenye urefu wa Kilomita 3 pamoja na barabara
unganishi zenye urefu wa km 1.66 huku ikigarimu shillingi Billioni 718.
Uzinduzi wa daraja hili la kimkakati unaendeleza adhma ya Rais
Samia katika kuchochea maendeleo ya mikoa ya Kanda ya Ziwa hususani mikoa ya
Mwanza,Geita,na Kagera Kiutalii na Kiuchumi.
Akizungumza na wanahabari baada ya uzinduzi wa Daraja hilo
Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji alisema kuwa kuzinduliwa kwa
daraja hilo linakwenda kuboresha mazingira ya biashara hususani biashara ya
usafirishaji na utalii wa Kanda ya Ziwa hususani katika Hifadhi za Taifa Kisiwa
cha Rubondo, Kisiwa cha Saanane , Hifadhi ya Taifa Burigi - Chato, Rumanyika
-Karagwe na Ibanda - Kyerwa.
"Daraja hili la JP Magufuli linaenda kuongeza ufanisi zaidi
katika utalii wa Kanda ya Ziwa na maendeleo ya biashara. Awali wageni katika
Hifadhi za Kanda ya Ziwa walitumia muda mrefu kusubiri vivuko ili kuyafikia
maeneo ya Hifadhi za Taifa zilizopo
katika mikoa ya kanda ya ziwa adha ya kusubiri vivuko kwa lisaa limoja mpaka
mawili sasahivi imekwisha.”
“TANAPA tunapenda kumshukuru Rais Samia kwa namna ambavyo
anaipambania sekta ya utalii.
Uwepo wa daraja hili ni kete nyingine kwa Utalii wa Nchi yetu
hususani Kanda ya Ziwa, tumeshuhudia Royal Tour na Amazing Tanzania na sasa
Rais anaboresha miundombinu ya Barabara ambazo ni nyenzo muhimu katika Utalii”
alisema Kamishna Kuji.
Serikali ya Awamu ya Sita imeendeleza adhma ya kuboresha
miundombinu ya Barabara ambapo imetekeleza ujenzi wa madaraja mengine makubwa
(9) ikiwemo daraja la Tanzanite - Dar es Salaam.
Na. Edmund Salaho - Busisi, Sengerema
0 Maoni