Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA) imeendelea kutumia fursa ya maadhimisho ya wiki ya utumishi
wa umma yanayoendelea Jijini Dodoma katika Viwanja vya Chinangali park,
kuhamasisha utalii wa ndani kwa wananchi na wadau mbalimbali waliofika kwenye
banda la NCAA ndani ya Banda la Wizara ya Mali Asili na Utalii.
Wananchi waliofika
kwenye banda hilo, wamesikika wakisifia huduma inayotolewa na wataalam wa
Mamlaka hiyo hususani, vivutio vilivyopo ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro
huku wengi wao wakionekana kufurahia kupata uwelewa kuhusiana na vivutio hivyo
na wengine wamekiri kuwa walikuwa hawajui historia na upekee wa eneo hilo
lilosheheni vivutio vilivyobeba historia ya pekee duniani.
"Nimejisikia
fahari kujua Tanzania tumebeba Historia adhimu Duniani ya Chimbuko la
Mwanadamu, huu ni urithi mkubwa sana, natamani mimi na familia yangu tufike
Laitole nikajione masalia hayo ya nyayo". Alisema Bi. Theresia Steven
mmoja wa wakazi wa Dodoma aliyetembelea banda la NCAA.
Maadhimisho ya Wiki
ya Utumishi wa Umma yaliyoanza tarehe 16 Juni 2025 yanatarajiwa kufikia kilele
chake kesho tarehe 23 Juni 2025, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa (Mb).
0 Maoni