Afisa Elimu, Kazi na
Jinsia kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Bwana
Nsubisi Mwasandende, ameipongeza Tume ya Madini kwa juhudi kubwa inazozifanya
katika kusimamia rasilimali za madini nchini na kuongeza mchango wake katika
Pato la Taifa.
Akizungumza katika
maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma,
Mwasandende amesema kuwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye uchumi wa nchi
umeendelea kuongezeka kwa kasi.
“Ripoti za hivi
karibuni zinaonyesha kuwa Sekta ya Madini imechangia zaidi ya asilimia 10 ya
Pato la Taifa (GDP). Hili ni jambo la kujivunia na nawapongeza sana Tume ya
Madini kwa kazi nzuri wanayoifanya, amesema.
Kwa upande wake,
Mhandisi wa Migodi, Bi. Colliness Seiya, ameeleza kuwa Tume ya Madini imefanya
maboresho makubwa kwenye mfumo wa utoaji wa leseni kwa lengo la kuongeza uwazi,
uwajibikaji na ufanisi wa shughuli za uchimbaji wa madini.
“Mfumo wa sasa wa
utoaji wa leseni umejengwa kidijitali kupitia Online Mining Cadastre
Transactional Portal (OMCTP), ambapo waombaji wanatuma maombi yao mtandaoni.
Hii imepunguza urasimu na kutoa nafasi kwa uwazi zaidi katika mchakato wa
maombi,” amesema Mhandisi Colliness.
Aidha, ameeleza kuwa
mfumo huo unawawezesha waombaji wa leseni za utafutaji au uchimbaji wa madini
kufuatilia hatua zote za maombi yao kwa njia ya mtandao bila ya kulazimika
kufika katika ofisi za serikali.
“Hii imeongeza
ufanisi na kupunguza malalamiko ya upendeleo. Kila hatua inaonekana wazi na kwa
wakati,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Sheria
ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake, Tume ya Madini inatoa aina
mbalimbali za leseni kulingana na shughuli husika, ikiwemo:
• Leseni ya Utafutaji wa Madini (Prospecting Licence)
• Leseni ya Uchimbaji Mdogo (Primary Mining Licence)
• Leseni ya Uchimbaji wa Kati na Mkubwa (Mining Licence na
Special Mining Licence)
Mhandisi Colliness
amebainisha kuwa kumekuwa na ongezeko la maombi ya leseni kutokana na
kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuendesha
shughuli za madini kwa kuzingatia sheria na taratibu.
Aidha, utoaji wa
leseni kwa uwazi umewezesha ukusanyaji madhubuti wa mapato ya Serikali kupitia
ada na tozo mbalimbali, utunzaji wa mazingira na usimamizi wa haki za jamii
katika maeneo ya uchimbaji.
“Mfumo huu si tu
umesaidia kuongeza mapato ya Serikali, bali pia umekuwa chombo muhimu cha
kuhakikisha mazingira na jamii zinazozunguka maeneo ya madini zinalindwa
ipasavyo,” amehitimisha.
0 Maoni