KATIBU Mtendaji wa
Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo, na Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na
Utawala, Nsajigwa Kabigi, wametembelea banda la Tume ya Madini katika
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayohitimishwa leo katika viwanja vya
Chinangali, jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo,
viongozi hao wamejionea namna Tume ya Madini inavyoshiriki kikamilifu katika
utoaji wa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake, huduma mbalimbali zinazotolewa
na mafanikio yaliyopatikana katika usimamizi wa rasilimali za madini nchini.
Mhandisi Lwamo
sambamba na kuwapongeza wataalam waliopo kwenye banda hilo, amewataka kuendelea
kutoa huduma kwa weledi, uwazi na
ubunifu kwa kuzingatia mabadiliko ya kidijitali ili kuwawezesha wananchi
kupata taarifa kwa haraka na kwa usahihi.
Kaulimbiu ya mwaka
huu ni: “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijitali ili Kuongeza Upatikanaji wa
Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji”, ambayo inalenga kuimarisha utendaji katika
utumishi wa umma kupitia matumizi ya teknolojia.
Maadhimisho haya
yanahitimishwa leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), ambapo taasisi mbalimbali za serikali zimepata
fursa ya kuonesha huduma wanazotoa na jinsi zinavyowahudumia wananchi kwa
uwazi, uwajibikaji na ubunifu.
Tume ya Madini
imeendelea kuwa taasisi muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kupitia usimamizi
endelevu wa Sekta ya Madini, huku ikiendelea kuboresha huduma kwa kutumia
mifumo ya kidijitali kwa maendeleo jumuishi ya Taifa.



0 Maoni