Mgombea urais nchini
Colombia, Seneta Miguel Uribe Turbay (39), amelazwa hospitalini akiwa mahututi baada ya kupigwa risasi mara tatu,
ikiwemo mara mbili kichwani akiwa kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika
Jumamosi katika bustani moja jijini Bogotá.
Kwa mujibu wa taarifa
kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, kijana mwenye umri wa miaka 15 alikamatwa
katika eneo la tukio na anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusiana na
shambulio hilo.
Mke wa seneta huyo,
Maria Claudia Tarazona, amewaomba wananchi wa Colombia kuungana kwa maombi kwa
ajili ya uzima wa mumewe. “Miguel kwa sasa anapigania maisha yake. Tumwombe
Mungu awaongoze madaktari wanaomhudumia,” alisema Tarazona kwa uchungu.
Chama chake cha
Centro Democrático kimelaani vikali tukio hilo, kikieleza kuwa ni tishio kwa demokrasia
na uhuru nchini humo.
Video iliyorekodiwa
kwa simu na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha tukio la kupigwa
risasi wakati Turbay akiwasilisha hotuba, hali iliyozua taharuki na kusababisha
watu kukimbia kwa hofu.
Kwa mujibu wa shirika
la habari la AFP, wahudumu wa afya wamesema Turbay alipigwa risasi kwenye goti
na mara mbili kichwani. Alipelekwa hospitalini kwa helikopta ambapo wafuasi
wake walikusanyika kwa ajili ya sala na dua.
Meya wa Bogotá,
Carlos Fernando Galán, amesema Turbay amefanyiwa upasuaji na kwa sasa yuko
kwenye saa muhimu za awali za uangalizi akiwa mahututi.
0 Maoni