Ufalme wa Denmark umeweka wazi dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano wa karibu na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika nyanja za kisiasa, kiuchumi
na kidiplomasia, ili kuchochea maendeleo ya pamoja kati ya mataifa hayo mawili.
Hayo yamebainishwa Juni 5, 2025, katika hafla ya maadhimisho ya
Siku ya Katiba ya Denmark (Grundlovsdag) iliyofanyika kwenye makazi rasmi ya
Balozi wa Denmark nchini, jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilikuwa ni sehemu ya
kumbukizi ya miaka 176 tangu kutiwa saini kwa Katiba ya Denmark mwaka 1849 —
moja ya Katiba kongwe zaidi duniani.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo, ambaye
aliongozana na viongozi wa kibalozi, wawakilishi wa sekta binafsi, mashirika ya
maendeleo, asasi za kiraia na wanahabari.
Akihutubia wageni waalikwa, Balozi wa Denmark nchini Tanzania,
Mheshimiwa Jesper Kammersgaard, alisema kuwa taifa lake limechagua kuendeleza
uwepo wake wa kidiplomasia nchini Tanzania kama sehemu ya mwelekeo mpya wa sera
ya nje ya Denmark barani Afrika.
“Leo tunasema kwa kauli moja, Denmark
imerudi rasmi Tanzania,” alisema Balozi Kammersgaard huku akisisitiza umuhimu
wa ushirikiano wa kweli, wa kuaminiana na wenye misingi ya kuheshimiana.
Alibainisha kuwa Tanzania imepiga
hatua kubwa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, hasa katika ukuaji wa tabaka
la kati na maendeleo ya sekta za kilimo na biashara. Vilevile, aliipongeza
Serikali ya Tanzania kwa mwelekeo wake mpya wa sera za kigeni, hasa diplomasia
ya kiuchumi inayotoa nafasi kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika
maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Waziri Kombo
aliipongeza Denmark kwa kuwa mshirika wa muda mrefu na wa kuaminika wa
Tanzania, akieleza kuwa ilikuwa nchi ya kwanza kuanzisha rasmi ushirikiano wa
maendeleo na taifa hili. Aidha, alitambua mchango mkubwa wa Shirika la
Maendeleo la Denmark (DANIDA) katika kusaidia vipaumbele vya maendeleo ya taifa
hususan katika sekta za elimu, afya, maji, na kilimo.
“Uhusiano wetu sasa umebadilika
kutoka kwenye msingi wa misaada ya maendeleo na kuwa ushirikiano wa maslahi ya
pamoja unaolenga biashara, uwekezaji na maendeleo ya watu,” alisema Kombo.
Kupitia mkakati wake mpya kwa
Afrika uitwao Karne ya Afrika, Denmark inalenga kushirikiana kwa
usawa na mataifa ya Afrika katika kukuza uchumi wa kijani, kuongeza biashara na
kuvutia uwekezaji. Mkakati huo pia unaweka msisitizo kwa mahusiano ya moja kwa
moja kati ya watu wa pande zote mbili.
Siku ya Katiba nchini Denmark
huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni, ikiwa ni kumbukumbu ya siku ambayo
Katiba ya mwaka 1849 ilisainiwa na hivyo kumaliza enzi ya utawala wa kifalme wa
mabavu. Katiba hiyo ndiyo msingi wa demokrasia ya Denmark hadi leo, ikilinda
haki za raia na usawa katika kushiriki mchakato wa kisiasa.
Wadau waliohudhuria hafla hiyo
walitumia nafasi hiyo kusisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa muda
mrefu kati ya Tanzania na Denmark, wakisema ni mfano bora wa mahusiano
yanayojengwa kwa misingi ya heshima, uaminifu na maendeleo ya pamoja.
0 Maoni