Serikali imeendelea
kutambua mchango wa walimu katika maendeleo ya sekta ya elimu kwani ni
wazalishaji wa watalaamu mbalimbali waliopo katika sekta zote ikiwemo afya,
nishati, sayansi na teknolojia. Sambamba na kufanya maboresho yatakayowaongezea
walimu ari ya kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na kutanguliza mbele
maslahi ya Taifa.
Mafanikio
yaliyopatikana katika sekta hiyo yanachangiwa moja kwa moja na walimu. Hivyo,
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kina mchango mkubwa kwa jamii na kwa Taifa kwa
ujumla kwa kuwa pamoja na jukumu la kufundisha na kujengea watu maarifa,
mwalimu ni mzazi wa kiroho, kiongozi wa fikra, na ni mjenzi wa maadili katika jamii.
Hayo yameelezwa na
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko Juni 8, 2025
jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama
Cha Walimu Tanzania (CWT).
Amesema katika
kuimarisha sekta ya elimu ili kuongeza ufanisi na kusogeza huduma kwa jamii.
Serikali imefanikiwa kujenga jumla ya madarasa 62,685 kwa shule za msingi na
sekondari, shule mapya za sekondari 1,031, shule mpya za msingi 1,580 na nyumba
za walimu 1,792.
Ameongeza kuwa katika
kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2024/25, Serikali imefanikiwa kuwalipa
malimbikizo ya mishahara walimu 101,596, kulipa watumishi 156,556 madeni yasiyo
ya mishahara na kuongeza mshahara kwa watumishi wa umma ambapo kima cha chini
kuanzia mwezi Julai, 2025 kitakuwa shilini 500,000 badala ya 370,000.
“Serikali inaendelea
kutoa ajira za walimu ambapo kuanzia mwaka 2021 hadi sasa, jumla ya walimu
40,527 wameajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini. Lengo la kufanya hivi ni
kutatua changamoto mbalimbali zilizopo,” amesema Dkt. Biteko.
Amepongeza matokeo ya
zoezi la ‘Samia Teachers Mobile Clinic’
kwa kuwafikia walimu 48,380 pamoja na kutatua kero zao huku akiwaomba
kuongeza ubunifu utakaowawezesha kuwa na mikakati mingine yenye lengo la
kuimarisha utendaji katika sekta ya elimu na kushirikiana na Serikali kwa
kutekeleza miradi ya Elimu ya TEHAMA kwa walimu na miradi mingine isambae kwenye mikoa yote nchini.
Kuhusu ombi la walimu
kuwa na mwajiri mmoja anayeshughulikia masuala yote ya walimu ili kuimarisha
ufanisi katika kuwasimamia. Dkt. Biteko amesema Serikali imelipokea ombi hilo
na italifanyia tathmini ili kubaini endapo utaratibu uliopo sasa una changamoto
zinazolazimu kutatuliwa kwa kuanzisha chombo kitakachosimamia walimu wote
nchini.
Amezungumzia
utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa na kusema kuwa lengo lake ni kukuza elimu
inayotolewa nchini na kuwafanya wanafunzi waweze kujitegemea wanapomaliza
masomo yao. Aidha, Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa
walimu wote wanapata mafunzo ili waweze kuendana na mabadiliko hayo.
Fauka ya hayo,
kufuatia kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa CWT, amewasihi wajumbe wa
Mkutano huo kutumia haki yao katika kuchagua viongozi watakaowaongoza vyema na
kuwataletea maendeleo pamoja wagombea
kuomba kura kwa heshimiana.
“ Nawasihi kuendelea
kusimamia misingi ya haki, usawa na uwazi hususan wakati wa majadiliano na
utatuzi wa masuala yote yanayohusu chama chenu. Niwaombe watakaoshinda
msiwanange watakaoshindwa na mtakaokosa nafasi msikasirike, asitokee mtu wa
kuwagawanya, msigawanyike hii ni taalamu ya pili ya uumbaji, mshikamane,
mpendane na mshirikiane,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Naye, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwan
Kikwete amesema kuwa Serikali inathamini mchango wa walimu katika mipango
mbalimbali ya Taifa na kuahidi kuendeleza ushirikiano mzuri kwa ajili ya ujenzi
wa Taifa na uchumi imara.
Kupitia mkutano huo,
Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania, Leah Ulaya amempongeza Rais Samia kwa
utendaji kazi wake na kuahidi kuwa CWT itaendelea kushirikiana na Serikali.
Naye, Kaimu Katibu
Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Joseph Misalaba ameishukuru Serikali
kwa kuendelea kulipa stahiki mbalimbali za walimu ambapo walimu wamenufaika kwa
kupandishwa vyeo, ulipwaji wa malimbikizo ya mishahara na madeni yasiyo ya
mishahara.
“ Kwa niaba ya
watumishi wa Tanzania hususan walimu wote tunaipongeza Serikali ya Awamu ya
Sita kwa kusikiliza kilio cha wafanyakazi juu ya suala la kikokotoo cha mafao
ya kustaafu na kuridhia kuboresha kikokotoo kutoka asilimia 33 hadi asilimia
40. Chama cha Walimu Tanzania kinaiomba Serikali yako iendelee kufanya
maboresho zaidi ili kuleta ustawi wa walimu wetu wastaafu ambao wameitumikia
nchi yao kwa uaminifu mkubwa,” amesema Misalaba.
Amefafanua kuwa CWT
ni chama cha wafanyakazi ambacho msingi wake mkubwa ni kutetea haki na maslahi
ya wanachama wake. Kama mdau wa elimu CWT itaendelea kushirikiana na Serikali
na wadau mbalimbali wa elimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu
nchini.
Aidha, Mkutano huo wa
mwaka wa CWT umehudhuriwa pia na wawakilishi wa vyama vya walimu kutoka nchi za
Rwanda, Burundi, Afrika Kusini na Namibia.
Na. Ofisi ya Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni