Matumizi ya TEHAMA yaongeza ufanisi na mapato NHC

 

Katika kuhakikisha linaendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha mifumo ya kidijitali inayoboresha huduma kwa wateja wake na kuongeza ufanisi wa ndani ya shirika.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo mapema wiki hii, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah Hamad, amesema kuwa tangu mwanzo wa mwaka 2021, Shirika lilianzisha utengenezaji wa mfumo wa kisasa unaojulikana kama “NHC Integrated System – NHC IS”, uliobuniwa na kutengenezwa na wataalamu wa Kitanzania kwa usimamizi wa karibu wa Kitengo cha TEHAMA cha Shirika.

“Mfumo huu ni wa kidijitali, jumuishi na unaziunganisha shughuli muhimu ndani ya Shirika kwa ufanisi mkubwa. Mpaka sasa mfumo huu umeunganishwa moja kwa moja na mfumo wa malipo ya Serikali – GePG pamoja na mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya usimamizi wa taarifa za Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT),” alisema Bw. Hamad.

Ameeleza kwamba mfumo huo unamuwezesha kujua kila kinachoendelea ndani ya NHC hata akiwa nyumbani kwake, lengo sasa ni kuuboresha zaidi kwa kutumia akili unde (AI) ili uweze kuwa na uwezo wa kutoa ripoti.

Pia, Bw. Hamad amesema kwa sasa mipango inaendelea ili kuunganisha mfumo NHC Integrated System – NHC IS  na mifumo mingine ya Serikali na taasisi mbalimbali kwa lengo la kurahisisha utoaji huduma na ufanisi wa kiutendaji kwa ujumla.

Aidha, Shirika hilo lipo katika hatua za mwisho kukamilisha “NHC Mobile App”, programu ya simu janja itakayowezesha wateja kuwasilisha maoni na kupata huduma mbalimbali kwa urahisi. Programu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi Julai 2025.

“App hii ya NHC Mobile App ni muhimu sana maana tunataka kumuwezesha mteja wetu popote pale alipo duniani kuweza kuangalia nyumba zetu tunazouza na kukodisha na kufanya maamuzi baada ya kujiridhisha,” alisema Bw. Hamad.

Aidha, NHC imechukua hatua kadhaa za kiteknolojia kuhakikisha usimamizi thabiti wa rasilimali na kupunguza udanyanyifu na kudhibiti wizi. Hatua hizi ni pamoja na usimikaji wa kamera za ulinzi (CCTV) kwenye miradi yote mikubwa pamoja na matumizi ya vifaa vya bayometriki kudhibiti malipo ya wafanyakazi kwenye miradi hiyo.

“Teknolojia hizi zimeleta mabadiliko chanya. Tumepunguza gharama za uendeshaji na kuongeza mapato ya Shirika kupitia usimamizi mzuri wa miradi ya ujenzi na udhibiti wa matumizi,” alisema Bw. Hamad.

Kwa ujumla, juhudi hizi zinathibitisha dhamira ya Shirika la Nyumba la Taifa kuendelea kuwa taasisi ya mfano katika matumizi ya teknolojia ya kisasa kwa lengo la kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Chapisha Maoni

0 Maoni