Serikali ya Iran imeongeza
marufuku ya kutembea na mbwa katika miji kadhaa nchini humo, ikitaja sababu za
usalama wa umma pamoja na afya ya wananchi. Hatua hiyo imeibua hisia mseto,
hasa miongoni mwa vijana wa mijini wanaoendelea kumiliki mbwa licha ya
vizingiti vinavyowekwa.
Kwa mujibu wa shirika
la habari la AFP, marufuku hiyo sasa inatekelezwa katika angalau miji 18,
zikiwemo Isfahan na Kerman. Marufuku hii ni mwendelezo wa agizo la polisi la
mwaka 2019 lililoweka katazo rasmi la kutembea na mbwa katika mji mkuu wa
Tehran.
Mbali na kutembea na
mbwa, kusafirisha wanyama hao kwa kutumia magari pia kumepigwa marufuku. Hii ni
kwa mujibu wa mamlaka zinazohusika na utekelezaji wa sheria, ambazo zinasema
hatua hiyo inalenga kulinda afya na usalama wa raia.
Tangu Mapinduzi ya
Kiislamu ya mwaka 1979, umiliki wa mbwa nchini Iran umekuwa ukitazamwa kwa
mtazamo hasi na mamlaka, ambazo zinawaona mbwa kuwa "wachafu" na
ishara ya ushawishi wa utamaduni wa Kimagharibi.
Hata hivyo, hali hiyo
haijazuia ongezeko la umiliki wa mbwa, hasa miongoni mwa vijana wanaoona
wanyama hao kama marafiki wa karibu na njia ya kuonesha upinzani dhidi ya
kanuni za utawala mkali wa Kiislamu.
Ingawa hakuna sheria
ya kitaifa inayokataza moja kwa moja umiliki wa mbwa, baadhi ya waendesha
mashtaka nchini humo wamekuwa wakitoa maagizo ya mitaa yanayotekelezwa
kikamilifu na vyombo vya dola.
Kwa sasa, hali hiyo
imezua mjadala mkubwa mitandaoni huku wananchi wakitafakari uhuru wao katika
maisha ya kila siku ukizidi kudhibitiwa na sera za kihafidhina.



 
 
 
 
 
 
 
 
0 Maoni