Katika safari ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, mchango wa taasisi za umma kupitia gawio na mapato mengine yasiyo ya kodi, ni chachu ya ustawi wa taifa.
Serikali imewekeza
jumla ya Sh86.3 trilioni katika taasisi za umma na kampuni ambazo ina umiliki
wa hisa chache.
Uwekezaji huu mkubwa
unaipa Serikali msingi wa kisheria na kiutendaji wa kudai mapato kutoka kwa
taasisi hizo kama sehemu ya kurejesha thamani ya uwekezaji wa umma.
Katika kutambua
umuhimu huo, Serikali imeanzisha Siku ya Gawio – itakayoadhimishwa Jumanne,
Juni 10, 2025 – kama sehemu ya kuenzi na kuhamasisha ushiriki wa mashirika ya
umma na kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache katika kuchangia maendeleo ya
taifa.
Kwa mujibu wa Msajili
wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, gawio na michango mingine ya mapato yasiyo ya
kodi huchangia moja kwa moja kwenye bajeti ya Serikali.
Fedha hizi husaidia
kugharamia huduma za msingi kama afya, elimu, maji safi na salama, pamoja na
ujenzi wa miundombinu muhimu inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Mapato haya,
yanayokusanywa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, huwasilishwa moja kwa moja katika
Mfuko Mkuu wa Serikali ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya
maendeleo.
Kwa kufanya hivyo, Serikali hupunguza
utegemezi wa misaada kutoka kwa wahisani na mikopo kutoka nje, hivyo kuimarisha
uhuru wa kifedha na kuwezesha maamuzi ya kisera yaliyojikita katika vipaumbele
vya kitaifa.
Katika kipindi cha
Serikali ya Awamu ya Sita, mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Ofisi ya
Msajili wa Hazina yameongezeka kutoka shilingi bilioni 637.67 mwaka 2020/21
hadi kufikia shilingi bilioni 767.2 mwaka 2023/24.
Hili ni ongezeko la
asilimia 20.3, linalothibitisha mafanikio ya juhudi za Serikali katika
kusimamia rasilimali za umma kwa weledi na kuongeza mchango wake katika bajeti
ya taifa.
Bw. Mchechu amesema
mwaka huu makubwa zaidi yategemewe, huku akisisitiza kuwa maandalizi
yamefanyika kikamilifu na taasisi nyingi tayari zimeonesha utayari wa kuchangia
zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Ili kufikia lengo la
mwaka huu wa fedha, ambalo ni kukusanya Sh1.113 trilioni. amehimiza kampuni,
taasisi na mashirika yote ya umma kuendelea kuwasilisha gawio na michango yao.
“Taasisi ambazo bado
hazijakamilisha kuwasilisha gawio na michango mingine zinatakiwa kufanya hivyo
kabla ya tarehe 30 Juni 2025,” aliagiza Bw. Mchechu.
“Ushirikiano wa kila
taasisi ni muhimu katika kuijenga Tanzania yenye uchumi imara, huduma bora kwa
wananchi, na maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.”
Aidha, utaratibu huu
wa uchangiaji huongeza uwajibikaji kwa mashirika ya umma, kwani unawalazimu
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kuimarisha utendaji wa ndani, na
kuhakikisha kuwa wanapata faida inayoweza kurejeshwa kwa umma kupitia gawio.
Idadi ya mashirika yanayotoa gawio na kiasi
kinachochangwa kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka, jambo linaloonesha
dhamira ya kweli ya taasisi hizi katika kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wa
kijamii, mapato haya huwezesha utekelezaji wa miradi yenye tija kwa wananchi
kama vile ujenzi wa vituo vya afya vijijini, madarasa, pamoja na huduma
nyingine za kijamii zinazoboreshwa kila mwaka kwa kutumia fedha zinazotokana na
gawio na michango mingine.
Kwa upande wake Bi
Lightness Mauki, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini -
Mashirika ya Kibiashara, Ofisi ya Msajili wa Hazina, alisema Kupitia uwazi
katika ukusanyaji na matumizi ya fedha, wananchi hujenga imani kwa taasisi za
umma na kupata ujasiri wa kufuatilia kwa karibu jinsi rasilimali za umma
zinavyotumika kwa manufaa ya wote.
Hali hii, aliongeza,
huongeza ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya maendeleo na kuimarisha
mshikamano wa kitaifa.
Ili kuimarisha zaidi
ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa
Hazina imeweka mikakati ya kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato kwa kutumia
mifumo ya TEHAMA kama PlanRep na mifumo ya malipo ya kielektroniki.
Aliongeza kuwa
Serikali pia imekuwa ikifanya tathmini za mara kwa mara za vyanzo vya mapato
ili kubaini fursa mpya za kuongeza mapato na kuhakikisha kuwa kila rasilimali
inatumika ipasavyo.
Vyanzo vya mapato
yasiyo ya kodi vinajumuisha gawio, ambalo hutokana na faida za mashirika na
taasisi za umma zinazofanya biashara.
Gawio hili hukusanywa
kwa mujibu wa Sheria ya Kampuni na Sheria ya Mashirika ya Umma.
Aidha, taasisi ambazo
hazimo kwenye kundi la gawio zinatakiwa kuwasilisha asilimia 15 ya mapato yao
ghafi kila mwaka kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma.
Pia, zipo taasisi zinazopaswa kuwasilisha mapato
ya ziada kila mwisho wa mwaka wa fedha, ambapo hulazimika kuwasilisha asilimia
70 ya ziada hiyo kwa Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina.
Vyanzo vingine ni
pamoja na marejesho ya mikopo na riba kutoka mashirika ya umma, pamoja na
mapato yanayotokana na matumizi ya mtambo wa TTMS unaosimamia mawasiliano ya
kielektroniki kati ya Tanzania na mataifa mengine.
Kwa upande wake Bi.
Neema Musomba, Mkurugenzi wa Huduma za Kimenejimenti alisema makusanyo yasiyo
ya kodi ni mhimili muhimu wa utekelezaji wa bajeti ya Serikali na miradi ya
maendeleo ya taifa.
Kwa kutambua hilo,
alisema, usimamizi wa mashirika ya umma umeimarishwa kwa kuhakikisha kuwa kila
taasisi inatekeleza wajibu wake wa kutoa gawio na michango mingine kwa mujibu
wa sheria.
“Ni wajibu wa kila
taasisi ya serikali, na kampuni ambayo serikali ina umiliki wa hisa,
kuhakikisha inashiriki katika kufanikisha ustawi wa taifa letu,” alisema Bi.
Musomba.
Kupitia kampeni ya
Siku ya Gawio 2025, Serikali inasisitiza umuhimu wa usimamizi bora wa
rasilimali za umma, uwajibikaji wa taasisi, na ushiriki wa kila shirika katika
kuchangia maendeleo ya taifa.
0 Maoni