Mamia ya washiriki
kutoka ndani na nje ya nchi wameshiriki msimu wa tano wa West Kili Forest Tour
Challenge 2025, tamasha la michezo na utalii lililolenga kuhamasisha uhifadhi
wa mazingira na uwekezaji kupitia utalii wa ndani.
Tamasha hilo
lililofanyika Juni 21 hadi 22 kwenye misitu ya West Kilimanjaro, wilayani Siha,
limeelezwa kuwa jukwaa linaloimarisha biashara, burudani, na mshikamano wa
kijamii kupitia michezo ya mbio, baiskeli na pikipiki.
Akizungumza wakati wa
kilele cha tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Godfrey Eliakimu Mnzava,
ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
(TFS) kwa ubunifu wa kuunganisha michezo, utalii na uhifadhi wa mazingira.
“Vivutio na juhudi za
uhifadhi zinazofanyika West Kilimanjaro ni za kipekee. Tukio hili linatoa
hamasa kwa utalii wa ndani na kuwavutia pia wageni kutoka nje kuona uzuri wa
rasilimali tulizonazo,” alisema Mnzava.
Alisema juhudi hizo
zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa kupitia sekta ya utalii, na
kusisitiza umuhimu wa kuunga mkono sera ya Rais ya kufungua fursa za utalii na
uwekezaji.
“Leo tumeshuhudia
burudani, michezo na watu wakifurahia. Ni tukio lisilopaswa kukosa. TFS
nawapongeza kwa ubunifu huu mkubwa,” aliongeza.
Mkuu wa Wilaya ya
Siha, Dkt. Christopher Timbuka, aliwahimiza Watanzania kushiriki kikamilifu
matukio ya aina hiyo badala ya kuamini kuwa utalii ni kwa wageni pekee.
“Utalii si kwa wageni
tu. Ni fursa ya kujifunza, kuburudika, na kupata elimu kuhusu uhifadhi. Nawaomba
Watanzania, hususan waishio maeneo ya jirani, wajitokeze kwa wingi msimu ujao,”
alisema.
Mhifadhi wa Shamba la
Miti West Kilimanjaro, PCO Robert Faida, alisema West Kili Forest Tour
Challenge imekuwa jukwaa linalounganisha biashara, michezo na uhifadhi, huku
idadi ya washiriki ikiongezeka kila mwaka.
“Utalii ni ajira.
Mwaka huu tumeshuhudia zaidi ya washiriki 200 kutoka ndani na nje ya nchi
wakishiriki katika mbio na mashindano ya baiskeli na pikipiki,” alisema huku
akisisitiza kuwa tukio hilo hutoa kumbukumbu chanya kwa kila mshiriki na
kusaidia kutangaza vivutio vya West Kilimanjaro.
Mkuu wa Dawati la
Utalii wa TFS, PCO Someni Mteleka, alisema tukio hilo ni sehemu ya makati wa
kukuza utalii wa misitu, ambapo asilimia 80 ya watalii wanaotembelea misitu ya
TFS kwa sasa ni Watanzania.
“Mbali na West
Kilimanjaro, mwezi Agosti tutakuwa na tukio la aina hii Msitu wa Rau, kisha
Rubare, Magamba na mashamba ya miti Morogoro,” alisema Mteleka.
Alifafanua kuwa tangu
2021 idadi ya watalii imeongezeka kutoka 59,000 hadi zaidi ya 280,000 kwa
mwaka, huku mapato yakipanda kutoka Sh milioni 154 hadi zaidi ya Sh bilioni 2.
“Dhamira yetu ni
kufikia watalii 500,000 kwa mwaka na mapato ya Sh bilioni 5. Mafanikio haya
yanatokana na uboreshaji wa miundombinu, ushirikiano wa wadau na ubunifu wa
matukio kama haya,” aliongeza.
0 Maoni